Na Fidelis Butahe, Mwananchi
SHARE THIS STORY
Dar es Salaam. Msiba wa Mbunge wa Mbinga
Magharibi, Kapteni John Komba jana uligeuka uwanja wa siasa, baada ya
makada wa CCM wanaotajwa kugombea urais pamoja na wapambe wao kupigana
vikumbo na kurushiana vijembe, ikiwa na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba.
Ilikuwa kama walijipanga kwani kila mgombea
aliyekuwa anafika katika msiba huo alionekana kuwa na wapambe
waliompokea, kumpeleka kutoa pole kwa wafiwa na kumuonyesha eneo la
kukaa.
Ukiacha kauli mbalimbali walizotoa kumwelezea
marehemu Komba (61), wapambe wa wagombea hao walionekana mara kwa mara
kuwa karibu nao wakizungumza, hali iliyoonyesha kuwa kila kundi lilitaka
mgombea wao kuonyesha uwepo wake.
Waliohudhuria
Wanaotajwa kuutaka urais ambao walihudhuria msiba
wa mbunge huyo uliotokea juzi jioni ni Mbunge wa Monduli, Edward
Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Songea Mjini, Dk
Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, wote kutoka
CCM, pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa.
Wapiga picha na Membe
Membe ndiyo alikuwa wa kwanza kufika nyumbani kwa
marehemu eneo la Mbezi Tangi Bovu na baada ya muda aliwasili Rais Jakaya
Kikwete na kukaa naye.
Mara baada ya Rais Kikwete kuondoka, Membe
alilakiwa na kundi kubwa la makada wa CCM ambao mbali na kumsalimia
walimvuta pembeni na kuomba kupiga naye picha huku wakisika wakisema
kuwa “Tunataka kupiga picha na mheshimiwa rais”.
Watu hao ambao walikuwa wakiongozwa na Mbunge wa
Tabora Mjini, Ismail Aden Rage ambaye hata hivyo hakupiga picha na
waziri huyo, walisema kuwa kama mambo yakienda vyema, Membe anaweza kuwa
rais na hata alipokuwa akiondoka walimsindikiza hadi kwenye gari lake.
Vijana na Nchimbi, Ngeleja
Ukiacha Dk Nchimbi ambaye alikuwa akizongwa zaidi
na vijana wa CCM, kivutio kingine kilikuwa kwa Ngeleja ambaye mara kwa
mara alikuwa akizungukwa na vijana waliokuwa wakimuuliza maswali
mbalimbali, hasa kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Ngeleja pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka walipata mgawo wa
fedha kutoka katika akaunti hiyo na tayari wamehojiwa na Kamati Ndogo ya
Maadili ya CCM, huku Ngeleja akisubiri kesho kuhojiwa na Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo tayari imeshamuhoji Profesa
Tibaijuka.
0 comments:
Post a Comment