Na Julius Mathias, Mwananchi
SHARE THIS STORY
Dar es Salaam. Kanisa la Pentekoste Tanzania
Usharika wa Tandika, Manispaa ya Temeke limenusurika kuteketezwa kwa
moto. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita na mtuhumiwa
alikamatwa na kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Chang’ombe.
Kaimu Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke,
Kamishna Msaidizi (ACP), Zacharia Sebastian alisema mtuhumiwa huyo
atafikishwa mahakamani leo baada ya taratibu kukamilika.
Akizungumza na gazeti hili katika ofisi yake,
ambako ndiko moto huo ulianzia, Askofu wa Kanisa Jimbo la Temeke,
Raymond Noya alisema tukio hilo ni la kushangaza, kwani halikulenga
kuiba mali zilizokuwamo kwenye ofisi hiyo.
“Hili siyo suala la uhuni…naona inaweza kuwa ni
vita dhidi ya imani. Lengo lilikuwa ni kuchoma kanisa na siyo kuiba
vilivyomo. Kama unavyoona hakuna kilichoguswa wala jaribio la kuvunja
ama mlango au dirisha. Hili ni jaribio la pili kutokea,” alisema Askofu
Noya.
Kuhusu jaribio la kwanza alisema lilitokea Novemba
mwaka jana, lakini hakukuwa na madhara makubwa na kesi ilifikishwa
kituo cha polisi ingawa hadi leo haijafikishwa mahakamani kwa maelezo
kuwa upelelezi bado unaendelea.
Noya alisema kwa miaka miwili iliyopita kumekuwa
na matukio tofauti yanayokwaza huduma ya kanisa, kwani wakati mwingine
wamekuwa wakirushiwa mawe wakati wa ibada.
“Kanisa lina mlinzi, lakini kuna wakati huwa
anazidiwa. Tangu kanisa hili lilipoanzishwa mwaka 1997 ni miaka miwili
tu iliyopita ndipo mambo yameanza kubadilika. Tumekuwa na ushirikiano
mzuri na watu wanaotuzunguka kwa muda wote tuliokuwapo hapa,” alieleza.
Alphonce John, mkazi wa eneo lilipo kanisa
alishangazwa na tukio hilo na kusema hakutegemea vitendo vya uharifu wa
aina hiyo vinaweza kufanyika wakati huu.
“Wanapokuwa na sherehe watu wa mtaani huwa
tunaalikwa na tunaenda kujumuika nao kwa chakula. Hakuna ugomvi wowote
kati yetu. Hii inashangaza,” alisema John.
0 comments:
Post a Comment