Ofisi hiyo chini ya Fungu 21 imeomba kuidhinishiwa
kiasi cha Sh790,325,216,000 kwa ajili ya shughuli mbalimbali
zinazotekelezwa kupitia katika idara zake kati ya hizo zaidi ya Sh50
bilioni zikiwa ni kwa ajili ya safari na posho mbalimbali.
Itakumbukwa kuwa tangu kumalizika kwa uwasilishaji
wa bajeti za kisekta kupitia wizara za Serikali, Kamati ya Bunge ya
Bajeti imekuwa katika mashauriano na Serikali, kusaka fedha kwa ajili ya
utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo ilionekana kuwa ni
muhimu.
Katika mashauriano hayo, Serikali na kamati
zilikubaliana kukata asilimia nane ya fedha za matumizi mengine katika
kila wizara na kuchukua kiasi cha Sh2 bilioni kutoka Hazina maalumu ya
Serikali ili kupata Sh225.281 bilioni kwa ajili ya maeneo yaliyokuwa na
upungufu.
Wakati hayo yakiendelea mabilioni ya fedha
yametengwa kwa ajili ya kazi za idara zilizopo chini ya Hazina ambazo
kimsingi zinapaswa kufanywa na watumishi wa Serikali katika kazi zao za
kawaida bila kupewa malipo ya ziada.
Ufafanuzi wa matumizi ya fedha uliotolewa kwenye
Randama za Hazina unaonyesha kuwa baadhi ya fedha zimetengwa kwa jumla
tu, pasipo kuonyesha uhalisia wa matumizi yake.
Miongoni mwa maeneo yaliyotengewa kiasi kikubwa
cha fedha ni kile kinachoitwa malipo ya tuzo kwa watumishi, vifaa vya
nyumbani kwa baadhi ya wakurugenzi na wakuu wa idara, posho za vikao
maalumu na malipo kwa ajili ya kazi ambazo kimsingi ni wajibu wa idara
husika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda
na Biashara, Luhaga Mpina, alisema Serikali haijapunguza matumizi
mengineyo katika bajeti zake za mwaka wa fedha 2014/2015 kama
ilivyoahidi katika bajeti iliyopita.
Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa (CCM),
alisema Serikali iliahidi kupunguza matumizi mengineyo (OC) kwa kiasi
cha Sh283 bilioni katika mwaka wa fedha 2013/2014, lakini hakuna
ushahidi kwamba imetekelezwa.
“Ahadi hiyo ilitolewa kwa maandishi na Waziri wa
Fedha, lakini hadi mwaka mwaka huu wa fedha unaelekea mwisho hakuna
mchanganuo wowote unaoonyesha kupunguzwa kwa matumizi hayo,” alisema
Mpina na kuongeza: “Bunge lilihakikishiwa kuwa kuhamishwa kwa fedha hizi
na kupelekwa katika miradi ya maendeleo hakutaathiri utendaji wa
Serikali. Lakini cha kushangaza, bajeti iliyowasilishwa matumizi
mengineyo (OC) yameongezeka.”
Alisema wakati wa uwasilishaji wa maoni ya kamati
yake kuhusu Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2014/2015, kamati
ilihoji kwa nini kwa kipindi kirefu Serikali imeendelea kutetea matumizi
ya aina hii kuwa ni muhimu, lakini Serikali haijawahi kuleta mchanganuo
wa matumizi hayo (matrix) ili kuthibitisha umuhimu unaosisitizwa?
0 comments:
Post a Comment