Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na
waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, kuhusu uchaguzi wa Serikali za
Mitaa uliofanyia Jumapili iliyopita. Kulia ni Naibu Mkurugenzi wa habari
wa chama hicho, Abdul Kambaya. Picha na Rafael Lubava
Dar es Salaam. Mwenyekiti
Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe amesema
umoja huo utafanya tathmini ya maeneo ambayo wangeweza kushinda kwa
kusimamisha mgombea mmoja kila eneo ili kuwachukulia hatua viongozi
waliokiuka makubaliano hayo.
Wenyeviti wa umoja huo wa vyama vinne CUF, Chadema, NLD na NCCR Mageuzi,
walisaini makubaliano kadhaa ikiwamo kusimamisha mgombea mmoja
atakayeungwa mkono na Ukawa katika chaguzi zote kuanzia Serikali za
Mitaa mpaka uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Jumapili,
katika baadhi ya maeneo, kila chama kilisimamisha mgombea wake na
matokeo yake kuipa nafasi CCM kushinda.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema alisema viongozi wote kutoka
vyama hivyo waliohusika kukiuka makubaliano hayo watachukuliwa hatua za
kinidhamu.
“Tutafanya tathmini ambayo itatupatia picha halisi ya sababu
zilizochangia baadhi ya maeneo kukiuka makubaliano. Tutawachukulia hatua
za kinidhamu. Tunajua hawakuwa na maandalizi na muda wenyewe ulikuwa
hautoshi lakini tutaangalia kwa nini hali hiyo ilijitokeza,” alisema
Mbowe.
Mbowe alisema awali, viongozi wa ngazi za juu katika umoja huo walitoa
maagizo ambayo yalitakiwa kutekelezwa na wagombea wote wanaounda Ukawa.
“Hakuna mwanachama asiyejua kama umoja ni nguvu, kwa viongozi wa ngazi
za juu tunalifahamu hilo kwa kiwango kikubwa lakini hata ngazi za chini
wanatakiwa kulitambua hilo,” alisema.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema changamoto hiyo
imekuwa kikwazo ambacho kimesababisha kukosa ushindi katika maeneo mengi
ya uchaguzi huo.
Nyambabe alisema tathmini itakayofanyika ndani ya umoja huo, itakuwa
nafasi muhimu ya kujipanga kufanikiwa katika uchaguzi mkuu ujao.
0 comments:
Post a Comment