Kikwete amkubali kujiuzulu
Jaji Werema alijiuzulu jana kupitia barua yake aliyomwandikia Rais Kikwete, akiomba kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo.Taarifa iliyotolewa jana usiku na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilisema:
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, amejiuzulu nafasi yake hiyo kuanzia leo (jana) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amekubali ombi hilo la kujiuzulu.”
Taarifa hiyo ilieleza kuwa katika barua yake kwa Rais Kikwete, Jaji Werema alisema kuwa ameomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusiana na suala ya Akaunti ya Tegeta Escrow hakueleweka na umechafua hali ya hewa.
“Mheshimiwa Rais Kikwete amemshukuru Jaji Werema kwa utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na uadilifu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo fupi.Sakata la wizi wa fedha hizo liliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi, David Kafulila, katika mkutano wa Bunge la Bajeti mwaka huu, lakini serikali ilikanusha kuchotwa kwa fedha hizo kwa maelezo kuwa hazikuwa za umma.
Miongoni mwa viongozi waandamizi wa serikali waliotoa kauli za kupuuza hoja ya Kafulila ni Jaji Werema na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Jaji Werema alivutana na Kafulila kuhusiana na sakata hilo na kutoleana maneno makali, huku Jaji Werema akitishia kumpiga Kafulila, na ugomvi huo ulisuluhishwa na baadhi ya wabunge na mawaziri ndani ya Bungeni.
Kabla ya kutaka kumpiga, Jaji Werema alimuita Kafulila kuwa ni tumbili na Kafulila alijibu mapigo hayo kwa kumuita Jaji Werma kuwa ni mwizi.
Kutokana na shinikizo hilo, Waziri Mkuu alimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi katika akaunti hiyo na kuwasilisha taarifa hiyo bungeni.
Aidha, Waziri Mkuu aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza tuhuma hizo.
Katika mikutano ya Bunge ya 16 na 17 iliyomalizika Novemba 29, mwaka huu, wabunge walishinikiza serikali kuhakikisha kwamba ripoti ya CAG inawasilishwa bungeni na kujadiliwa.
Baada ya mvutano huo, ripoti hiyo iliwasilishwa katika Ofisi ya Spika na baadaye kukabidhiwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
Zitto na Makamu wake, Deo Filikunjombe waliwasilisha ripoti hiyo bungeni na kuzua mjadala mkubwa.
Kamati hiyo ilipendekeza baadhi ya vigogo kufutwa kazi wakiwamo Waziri Mkuu Pinda, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu, Eliakim Maswi; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.
WEREMA ALIVYOSHIRIKI ESCROW
Wakati PAC ilipokuwa imejichimbia Dodoma kuchambua ripoti ya uchunguzi ya CAG, kulikuwa na ushahidi ulioonyesha jinsi Werema na Maswi, walivyohusika kumuamuru Gavana wa BoT, Beno Ndulu, aidhinishe uchotaji wa fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow kwenda IPTL.
Akaunti hiyo ilikuwa imefunguliwa BoT ili kuhifadhi fedha zilizokuwa zinabishaniwa kati ya Tanesco na IPTL.
Jaji Werema alidaiwa kuandika barua Oktoba 2, mwaka 2013 yenye Kumbukumbu Namba AGCC/E.80/6/65 kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha (Hazina), Dk. Servacius Likwelile, akitaka fedha hizo zitolewe haraka.
Walioiona barua hiyo wanasema kuwa Jaji Werema aliinakili barua hiyo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Katika barua hiyo Jaji Werema alinukuliwa akibariki kuchotwa kwa fedha hizo kwa msingi wa maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu chini ya Jaji John Utamwa.
Habari zilieleza kuwa kwa mujibu wa barua ya Jaji Werema, maamuzi ya kuidhinisha kuchotwa kwa fedha hizo yanalindwa na maamuzi ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Utamwa.
Katika barua hiyo, Jaji Werema alinukuliwa akifafanua kwamba, aliisoma ripoti na kuwa suala ambalo lilioonekana kuishughulisha timu iliyohusika, ni uwekezaji wa fedha za Escrow.
Ilielezwa kuwa Jaji Werema alisisitiza kuwa Akaunti ya Escrow ilikuwa ni zao la makubaliano juu ya akaunti ya Tegeta Escrow yaliyofanyika Julai 5, 2006, huku akiirejea kuwa BoT kama wakala wa Escrow, iliruhusiwa kuziwekeza fedha hizo kwenye “uwekezaji ulioruhusiwa” kama inavyoelekezwa kwenye kifungu cha 3.4 na 7.2 (c) cha makubaliano hayo.
Ilielezwa kuwa Jaji Werema katika barua yake alisema, njia sahihi na ya busara ni kwa wakala wa Escrow kuijulisha IPTL kuhusiana na uwapo wa “uwekezaji ulioruhusiwa” na lini utaiva.
Jaji Werema alikwenda mbali na kusisitiza kuwa, hakuna pingamizi lolote kuhusu IPTL kupewa fedha hizo kwa sababu tayari kulikuwa na hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa na Jaji Utamwa.
Alidaiwa kusema kuwa, uamuzi wa mahakama unalinda maslahi mapana ya umma dhidi ya malalamiko yasiyoisha juu ya fedha za akaunti ya Escrow.
Aidha, alidaiwa kusema kuwa ni maoni yake vile vile kwa wakala wa Escrow na serikali wazungumze na kukubaliana na IPTL juu ya nani anahusika na kukumbushia fedha hizo kabla hazijaiva kwa maslahi ya kampuni ili iendelee kufanya kazi.
Jaji Werema alinukuliwa akisema kuwa, udhamini wa serikali chini ya PPA ulikuwa umepitwa na wakati na kuonya kuwa serikali haiwezi kuwekwa kwenye hatari isiyotarajiwa kwa kuendelea kuhusika na fedha hizo.
Kadhalika, Jaji Werema alinukuliwa akipuuzia juu ya athari zinazoweza kutokea kutokana na kesi iliyofunguliwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) dhidi ya wamiliki wa IPTL kuwa haitakuwa na madhara juu ya uamuzi wa kuhamisha fedha hizo kutoka Escrow kwenda IPTL na kama ni mashitaka mapya atakayeshtakiwa ni IPTL wala siyo Serikali ya Tanzania.
WEREMA NI NANI
Jaji werema aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo baada ya kustaafu kwa mtangulizi wake, Johnson Mwanyika mwaka 2010, alipata shahada ya kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1984. Mwaka 1993 alipata shahada ya pili ya sheria kutoka Washington DC, Marekani.
Wakili na Mkurugenzi katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu mwaka 1984 hadi 2006.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania 2007-2009 Kung’oka kwa Werema kunawaachia mtihani wateule wengine wa Rais waliotajwa katika kashfa hiyo, Prof. Muhongo na Maswi pamoja na Profesa Tibaijuka ambaye alitajwa kupata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engneering Limited, James Rugemalira. VIP ilikuwa mwanahisa katika IPTL.
Ikulu Desemba 9, mwaka huu, ilitoa taarifa ikieleza kwamba Rais Kikwete atafanya maamuzi kuhusiana na sakata la Escrow wiki hii.
0 comments:
Post a Comment