RUSHWA NI TATIZO SUGU KATIKA NCHI YETU, NANI ATAWEZA KUIONDOA?

MWANDISHI Eric Shigongo
KATIKA kumuenzi Mungu, kila mtu ambaye leo afya yake ni nzuri hana budi kumshukuru na kumtukuza huku akimuomba awaponye wale wote walio katika magonjwa.

Baada ya kusema hayo nianze kwa kusema kuwa katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi, baadhi ya matawi wanachama wake wamelalamikia rushwa kwamba waliwapigia kura watu waliokuwa wanapenda kuwaongoza lakini kura zao zikachakachuliwa.

Nilisimuliwa kuhusu tawi moja eti waliochaguliwa waliiba kura na matokeo yakatajwa lakini baada ya msimamizi kupigwa na wanachama wenzake, kesho yake walioibiwa kura wakarudishiwa kura zao!
Wanachama hawakukubaliana na wizi huo na ikabidi sakata hilo lifikishwe ngazi ya wilaya.


Aliyeongoza katika uenyekiti akang’olewa lakini bado wanachama wanalalamikia wizi mkubwa uliofanyika katika kura za maoni kutokana na rushwa iliyotembezwa.

Hayo yametokea katika matawi mengi hapa nchini wakati wa kura za maoni. Hali hiyo si nzuri na inatoa changamoto mpya katika vita dhidi ya rushwa hasa kutokana na wananchi wengi kupoteza imani katika vita hiyo.

Wananchi ndiyo wanaoathirika moja kwa moja na rushwa na hawaoni hatua zozote madhubuti za kukomesha na kuwashughulikia watuhumiwa wa matukio hayo.Watanzania licha ya kuona matatizo hayo katika vyama vyao vya kisiasa, wamekuwa wakisumbuliwa na kulazimishwa kutoa rushwa wanapopata matatizo yanayohitaji huduma za kijamii hasa kwenye taasisi za umma ambazo zinaendeshwa na serikali kwa asilimia 100.

Watanzania pia wamekuwa wakiingia katika mtego wa kutoa rushwa baada ya kutembelea ofisi za serikali au watoa huduma katika sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali au ya dini katika maeneo yao.
Baadhi ya wananchi niliozungumza nao walisema waliwahi kuombwa rushwa na polisi, mahakimu au hata waliokuwa wakitafuta kazi.

Walisema polisi ndiyo wanaoongoza kwa kuomba rushwa.
Ukweli ni kwamba wananchi wamepoteza imani kabisa ya kupigana na rushwa kwa sababu hata zile kesi kubwa za rushwa zinazoibuliwa, mara nyingi zimekuwa zikipotelea hewani na hakuna anayewajibishwa.
Ni dhahiri hata Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (Takukuru) iliyopewa jukumu la kuchunguza, haijapewa meno ya kutosha.

Nashauri kwamba taasisi hiyo iwe na uwezo wa kusimamia uchunguzi na kuendesha kesi hizo yenyewe chini ya kiongozi wao Dk Edward Hosea.Kwa kutumia utafiti wa kipimo cha rushwa duniani wa 2013, uliofanywa na Shirika la Transparency International, Watanzania wamekuwa wakitoa rushwa mara nyingi zaidi kwa polisi.

Hata hivyo, wakati rushwa ikistawi nchini, Watanzania wengi hawana taarifa za kutosha na wengi hawajui kabisa kuhusu kashfa kubwa za rushwa zinazoelezwa katika vyombo vya habari.

Hili ni suala gumu lililoguswa katika ripoti ya utafiti huo na hadi matokeo yanatoka, asilimia zaidi ya 78 haikujua lolote kuhusu kashfa ya IPTL, asilimia 74 haijui lolote kuhusu kashfa ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati, David Jairo na asilimia 67 hawajui lolote kuhusu kashfa ya ununuzi wa rada.

Pia imegundulika kuwa asilimia 52 hawajui lolote kuhusu kashfa ya Epa na zaidi ya asilimia 44 hawajui lolote kuhusu kashfa ya Richmond.Wastani huo unashtua kwa sababu kwa idadi hiyo kubwa ya Watanzania wasiojua lolote kuhusu kashfa hizo kubwa za rushwa zinazowagusa moja kwa moja viongozi waandamizi serikalini, kunaonesha ni jinsi gani raia wasivyofuatilia mambo mazito.

Ukweli ni kwamba matatizo mengi ya nchi yanapata ‘kigugumizi’ katika kuyatatua hasa kashfa za rushwa kwa kuwa uelewa wa wananchi uko chini, licha ya kutangazwa na vyombo vya habari na kutawala mijadala ya kisiasa.

Katika utafiti huo, suala la rushwa katika sekta za usalama, siasa, kodi, ardhi, afya, elimu, maji, Serikali za Mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya dini, inawagusa zaidi ya asilimia 50 ambao wamefikia hatua ya kuiona kama ni kitu cha kawaida.

Wengi wamekuwa wakitoa rushwa wakiwa kwenye hali tete, hasa wanapokutana na polisi au wanapohitaji huduma za afya.Uombaji rushwa unaoshika nafasi ya pili ni ule unaowakabili wananchi wanapoomba ajira na sasa rushwa inatazamwa kama kitu cha kawaida kabisa.

Wakati wafadhili, wanasiasa na mashirika yasiyo ya kiserikali yakijikita kupambana na kashfa kubwa za rushwa, wananchi wengi wanaangalia zaidi aina ya rushwa inayowagusa moja kwa moja na kuathiri maisha yao ya kila siku.

Seriali chini ya Rais Jakaya Kikwete na wanasiasa wanaelekeza nguvu zao katika rushwa wanazoziita kubwa, ni sawa, lakini kutotilia maanani rushwa zinazowagusa wananchi moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku katika huduma za polisi, afya, elimu na ardhi ni kosa kubwa. Kiongozi gani atakabiliana na tatizo hili?

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli. GPL
SHARE

Milan Tomic

Hi. I’m Designer of Blog Magic. I’m CEO/Founder of ThemeXpose. I’m Creative Art Director, Web Designer, UI/UX Designer, Interaction Designer, Industrial Designer, Web Developer, Business Enthusiast, StartUp Enthusiast, Speaker, Writer and Photographer. Inspired to make things looks better.

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment