Tayari Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeshapuliza kipenga na kutangaza rasmi
tarehe ya uchaguzi huo kuwa ni Desemba 14, mwaka huu.
Katika uchaguzi huo, vyama ambavyo vimekuwa
vikipewa nafasi ya kuleta ushindani dhidi ya CCM katika uchaguzi huo ni
CUF, Chadema na NCCR Mageuzi kutokana na msingi wake wa mashina katika
ngazi za vijiji na vitongoji.
CCM imekuwa ikijigamba kuendeleza mtindo wake wa
ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo kwa kile inachodai kuwa na
mtandao imara tangu katika ngazi za chini kabisa yaani mashinani.
Nini sababu ya vyama vya upinzani kuonekana kushindwa kufurukuta mbele ya CCM.
Pamoja na ukweli huo wa kujijenga katika ngazi za
mashina, vyama hivyo vinalalamikia kuwepo kwa udhaifu mkubwa unaofanywa
na Serikali kwa makusudi ili kuipa CCM fursa ya kuendelea kuwa na nguvu
ya kuteka vijiji vingi nchini.
Nini kinaipa ushindi CCM
Samwel Ruhuza ni mdau wa masuala ya siasa. Amepata
kuwa katibu mkuu wa NCCR Mageuzi Bara. Anataja moja ya kigezo
kinachoipa CCM ushindi wa kishindo ni utaratibu uliopo wa uchaguzi huo
kufanyika chini ya ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inawakilishwa na
wakurugenzi wa halmashauri za wiyala nchini.
“Wakurugenzi wa halmashauri ndiyo wasimamizi wa
chaguzi hizo wanaowajibika kwa mkuu wa wilaya, ambaye ni mjumbe wa
Kamati ya siasa ya CCM wilaya, kwa mazingira hayo kwa hakika ni asilimia
ndogo sana CCM kukosa ushindi,” anasema na kuongeza:
“Mkuu wa wilaya ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
ya Wilaya anayetoa amri kwa mkuu wa polisi wa wilaya. Kwa hivyo CCM
wanaweza kucheza ‘rafu’ za wizi na wasichukuliwe hatua kwa agizo la mkuu
wa wilaya aliye na sura ya Mjumbe wa Kamati ya siasa (CCM).”
Ruhuza anatoa mfano wa hali iliyotokea Wilaya ya
Kasulu mkoani Kigoma mwaka 1999 kuwa chama chake cha NCCR Mageuzi
kilishinda katika vijijini vinane lakini Mkurugenzi wa halmashauri hiyo
kwa kipindi hicho aliamua kufuta matokeo hayo.
“Nakumbuka kijiji kimojawapo ni Mvungwe, baada ya
kunyang’anywa haki yetu tulikwenda mahakamani na kushinda mwaka 2003
ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kuingia uchaguzi mwingine 2004, licha ya
usumbufu tulioupata, ile ilitujenga kisiasa na kutusaidia kushinda
vijiji vyote uchaguzi uliofuata,” anaongeza Ruhuza.
0 comments:
Post a Comment