Na Sharon Sauwa na Fidelis Butahe, Mwananchi
Habari kutoka ndani ya kikao cha majadiliano baina
ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti zinasema, Sh11 bilioni
zimepunguzwa katika fungu hilo na kubakiza Sh39 bilioni.
Hata hivyo, kiasi kilichobakishwa ni ongezeko la
asilimia 260 la Sh15 bilioni zilizopitishwa na Bunge mwaka jana kwa
ajili ya safari za Rais katika mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30 mwaka
huu.
“Katika bajeti ya 2013/14 safari za Rais
zilitengewa Sh15 bilioni lakini inaonekana fedha zilizotumika ni nyingi
zaidi maana ndani ya miezi miwili tu zote zilikuwa zimemalizika,”
kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Kwa hiyo kwa mwaka 2014/15 Serikali ilimtengea
Rais Sh50 bilioni za safari, ila tumekata Sh11bilioni ili kupelekwa
katika shughuli nyingine za maendeleo. Kwa hiyo kwa mwaka ujao wa fedha,
safari za Rais zitatengewa Sh39 bilioni”.
Awali, ilielezwa kuwapo kwa mvutano mkali baina ya
Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti, lakini jana mchana pande hizo
zilikubaliana kukata asilimia 7.5 ya fedha katika baadhi ya mafungu ya
matumizi mengineyo (OC) kutoka katika wizara zote ili kuwezesha
kupatikana kwa Sh230 bilioni ambazo zinahitajika kwa ajili ya maendeleo
hasa katika sekta tatu; afya, miundombinu na kilimo.
“Bado kikao kinaendelea na tangu asubuhi tumekata
fedha katika fungu la matumizi mengineyo, mfano chai katika ofisi za
wizara pamoja na ununuzi wa magazeti, ununuzi wa magari ya kifahari,
mafuta, viburudisho, semina na makongamano pamoja na safari za ndani,”
kilieleza chanzo chetu.
Chanzo kingine kutoka Serikalini kilisema: “Katika
siku ambazo tumevutana kwenye kikao cha kamati ni leo (jana), lakini
mwishoni tulifikia mwafaka wa kukata kati ya asilimia saba na nane ya
fedha za matumizi mengineyo katika wizara zote, ili kupata fedha za
maendeleo.”
Juzi, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
alisema wizara yake inakusudia kupitia bajeti za wizara zote ili
kuhamisha fedha kutoka katika matumizi yasiyo ya lazima ili zielekezwe
katika mahitaji muhimu.
“Kama wananchi wanakula mlo mmoja kwa siku,
waliopo wizarani hawawezi kufa kwa kukosa chai asubuhi. Tutafanya hivyo
ili fedha hizo zipelekwe katika shughuli za maendeleo.
Kesho (jana) katika kikao cha mashauriano
tutakwenda kuweka msimamo wa pamoja katika jambo hilo. Wizara
zisielekeze macho Wizara ya Fedha pekee, nazo zinatakiwa kuwa na
mikakati ya kubana matumizi yake.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew
Chenge alipoulizwa kuhusu hatua iliyofikiwa katika majadiliano alisema:
“Subirini itakaposomwa bajeti mtajua kilichoamuliwa.”
0 comments:
Post a Comment