Na Joseph Zablon, Mwananchi
Posted Alhamisi,Novemba21 2013 saa 16:36 PM
Posted Alhamisi,Novemba21 2013 saa 16:36 PM
Watu hawajadili tena uchumi, kila mtu yupo kwenye siasa na hiyo imesababisha kutouza mifugo au nyama katika Falme za Kiarabu.
Katika vijiji vya Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani,
vurugu zimekuwa zikizuka mara kwa mara na kusababisha nyumba za baadhi
ya watendaji wa Serikali wakiwamo polisi kuchomwa moto.
Mali zinaharibiwa, watu wanapoteza maisha na wengine kubaki na ulemavu wa kudumu.
Ghasia hizo zinatajwa kusababishwa na kitendo cha
mfugaji mmoja kutoka Kanda ya Ziwa kuingiza mifugo yake katika shamba la
mkulima, mwenyeji wa eneo hilo na hata alipoulizwa, kulikoni, alipuuza.
Mkulima huyo hakukata tamaa, badala yake alikwenda polisi kutoa taarifa
ya mazao yake kuharibiwa na mifugo ambayo ilikuwa bado katika eneo la
tukio, lakini hakuna askari aliyemjali wala kumsikiliza.
Mkulima huyo alirudi mbio hadi kijijini kwake na
kuanza kupiga kelele za kuomba msaada, na kuwavuta wanakijiji wenzake,
wakakusanyika kila mmoja akiwa na zana za mapambano na ghasia kubwa
kuibuka.
Jeshi la Polisi lilitumia zaidi ya siku tatu
kuzima ghasia hizo na hivyo kuigharimu Serikali fedha nyingi katika
kuzima ghasia na gharama za matibabu.
Wakulima na wafugaji
Tikio hilo ni moja kati ya mengine mengi ambayo
yanatokea katika maeneo mbalimbali nchini baina ya wakulima na wafugaji,
ambayo yanawafanya wakulima kuwachukia wafugaji na kinyume chake.
Tanzania, ikiwa nchi ya tatu kwa wingi wa mifugo barani Afrika
ikitanguliwa na Sudan na Ethiopia, bado haijanufaika na mifugo hiyo.
Badala yake, mifugo hiyo inaonekana kuwa kero,
karaha na chanzo cha umaskini na uvunjifu wa amani kuliko kuwa neema,
furaha na chanzo cha utajiri.
Kwa wingi wa mifugo iliopo Tanzania, sekta hiyo
ingetarajiwa kuinufaisha nchi na watu wake kwa kiwango kikubwa, jambo
ambalo halijatokea.
Takwimu za karibuni za Wizara ya Mifugo na
Maendeleo ya Uvuvi zinaonyesha kuwa Tanzania ina ng’ombe milioni 22.8,
mbuzi milioni 15.6, kondoo milioni 7.0, kuku wa asili milioni 35.5, kuku
wa kisasa milioni 24.5 na nguruwe milioni 2.01.
Pamoja na mifugo hiyo, sekta hiyo imekuwa na
mchango finyu katika Pato la Taifa (GDP), kwani katika kipindi cha mwaka
2011 ilichangia asilimia 3.7.
0 comments:
Post a Comment