Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Ijumaa,Novemba22 2013 saa 8:32 AM
Posted Ijumaa,Novemba22 2013 saa 8:32 AM
Dar es Salaam. Suala la hatma
ya Naibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto
Kabwe ndilo lililotawala katika siku ya pili ya kikao cha Kamati Kuu ya
chama hicho na kusababisha mvutano mkali miongoni mwa wajumbe.
Pamoja na ukweli kuwa kulikuwa na ajenda kadhaa
zilizokuwa zimepangwa kujadiliwa katika kikao hicho cha siku mbili
kilichofanyika Dar es Salaam, suala la Zitto ndilo lililochukua muda
mrefu zaidi kujadiliwa.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho
zilieleza kuwa wajumbe waligawanyika makundi mawili, baadhi
wakipendekeza Zitto avuliwe nafasi yake ya Naibu Katibu Mkuu kwa maelezo
kuwa anakwenda kinyume na taratibu za chama hicho na wengine wakipinga
hatua hiyo kwa maelezo kuwa haina tija.
Mpaka saa moja usiku jana gazeti hili likienda
mitamboni, kikao hicho kilikuwa bado kikiendelea na suala hilo
lililokuwa chini ya ajenda ya hali ya siasa nchini.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa chama
hicho, Benson Kigaila aliahidi kuwa taarifa rasmi ya kikao hicho
ingetolewa baadaye na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Tuhuma za Zitto
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
mwanzoni mwa Novemba mwaka huu aliingia katika malumbano na Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho, akituhumiwa
na Lema kuwa anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho
kutoka mashirika mbalimbali nchini.
Pia, aliingia katika malumbano na chama chake
baada ya kutumia kofia yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC), kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake
hazikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kauli ambayo jana Kigaila aliitolea ufafanuzi na
kueleza kuwa Chadema kimekaguliwa na hesabu zake tayari zipo kwa Msajili
wa Vyama vya Siasa.
0 comments:
Post a Comment