YP kuzikwa leo makaburi ya Chang’ombe


Msanii wa kundi la muziki la TMK Wanaume Family, Yesaya Ambikile ‘YP’ 
Posted  Jumatano,Oktoba22  2014  saa 12:23 PM
Kwa ufupi
Kiongozi wa kundi hilo, Saidi Fella, alithibitisha kutokea msiba huo na kusema mazishi yatafanyika leo saa 10:00 katika makaburi ya Chang’ombe.
SHARE THIS STORY
0
Share
Dar es Salaam. Msanii wa kundi la muziki la TMK Wanaume Family, Yesaya Ambikile ‘YP’ amefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Temeke alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu ya kifua.
Kiongozi wa kundi hilo, Saidi Fella, alithibitisha kutokea msiba huo na kusema mazishi yatafanyika leo saa 10:00 katika makaburi ya Chang’ombe.
Alitaja sababu ya kifo cha msanii huyo kuwa ni maradhi ya kifua kikuu yaliyokuwa yanamsumbua kwa muda mrefu, ambapo alishaanza kunywa dawa na kufanya shughuli zake, lakini kwa bahati mbaya juzi akazidiwa na kupelekwa Hospitali ya Temeke na kufariki dunia usiku wa kuamkia jana.
Fella alisema marehemu ameacha mchumba aliyekuwa anaishi naye maeneo ya Ukonga jijini Dar es Salaam na mtoto wa kiume aitwaye Ambikile.
“Ninapozungumzia wasanii ambao nimewatengeneza mwenyewe, huyu ni mmojawapo. Nilimtangaza mwenyewe; nikamkuza; akaondoka kidogo katika kutafuta maisha, lakini baadaye alirudi kwa baba yake. La zaidi sina, namwombea Mungu apumzike kwa amani,” alisema Fella.
Fella alieleza jinsi alivyokutana na msanii huyu kabla ya kumwingiza katika Kundi la TMK Wanaume, akisema alikutana naye 2004 katika baa iliyokuwa ya King Palace maeneo ya Keko akiimba ‘free style’.
“Wiki hiyo hiyo nikiwa na Temba katika Baa ya Luxury Pub, Temeke nilimwona akifanya free style pia,” alisema Fella.
Alieleza kuwa alivutiwa na kipaji chake akamwita pembeni akamsikiliza na kumwita Temba naye akamsikiliza. Alikuwa na wimbo wake unaitwa “Saidali” na ndiyo wimbo wake wa kwanza .
Alisema baadaye walimwalika aende maskani ya kundi iliyokuwa Uwanja wa Taifa. Hapo akamwita na Juma Nature aende kumsikiliza ili kujiridhisha na kila mmoja alipoliridhika, wakamwingiza kundini.
“Kuanzia hapo nikamjumlisha kundini akawa msanii bora kabisa aliyeelewana na kila mtu na akifanya mambo yake kwa umakini na usikivu. Ndiyo maana nasema huyu ni sawa na mwanangu na yeye alikuwa ananichukulia kama baba yake,” alisema Fella.
Akizungumza kwa huzuni na gazeti hili kiongozi wa Kundi la Wanaume Halisi, Juma Nature alisema YP ni nyota iliyozimika ghafla. “Siamini kama tunachokizungumza sasa kinamhusisha YP, nahisi kama ni mashairi ya muziki wa huzuni kichwani mwangu, lakini hakuna jinsi, kazi ya Mungu haina makosa, ” alisema Nature.
Nature, ambaye aliwahi kufanya kazi katika kundi moja na marehemu, alisema cha msingi ni kumwombea apumzike kwa amani kwani hakuna aliyetarajia kama ugonjwa ule ungechukua uhai wake.
SHARE

Milan Tomic

Hi. I’m Designer of Blog Magic. I’m CEO/Founder of ThemeXpose. I’m Creative Art Director, Web Designer, UI/UX Designer, Interaction Designer, Industrial Designer, Web Developer, Business Enthusiast, StartUp Enthusiast, Speaker, Writer and Photographer. Inspired to make things looks better.

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment