Tukio hilo limejiri saa 2:30 usiku na bomu hilo
lilirushwa kwa mkono na watu wasiojulikana wakati waumini wakiagana na
mtoa mawaidha Sheikh Kassim katika eneo la kuegesha magari Darajani
visiwani Zanzibar.
Aliyefariki dunia kwa bomu hilo ametajwa ni Muhammed Khatib Mkombalaguha, ambaye ni mwanafunzi wa Sheikh Kassim.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai
Zanzibar (DDCI), Yusuph Ilembo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na
tayari Jeshi la Polisi limeanzisha operesheni maalumu ya kuwasaka watu
waliohusika na shambulio hilo kwa kushirikiana na vikosi vingine vya
ulinzi na usalama visiwani hapa.
“Mlipuko pia umesababisha magari mawili
yaliyokuwepo katika eneo la tukio kuathirika, ikiwemo kupasuka mipira na
gari lingine kuvunjika kioo, na tayari tumeanza kufanya uchunguzi
ingawa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa hadi hivi sasa,” alisema DDCI
Ilembo.
Alisema magari yaliyoathirika ni Toyota Prado
ambalo alikuwa akitumia Sheikh Kassim Mafuta tangu alipowasili visiwani
Zanzibar, Jumatatu ya wiki hii na kutoa mawaidha katika misikiti
mbalimbali ya kisiwani Unguja pamoja na Toyota IST.
Alisema katika eneo la tukio kumekutwa mabaki ya
mlipuko ambayo tayari yameanza kufanyiwa uchunguzi na wataalamu wa
mabomu, kubaini kama mabomu hayo ni ya kienyeji ama yalitengenezwa
kiwandani.
Aliwataja majeruhi ni Sheikh Kassim Mafuta, Kassim
Issa Muhammed (38) mkazi wa Fuoni, Hamad Nassor Kassim (46), Khelef
Abdallah Abdallah (21), Khalid Ahmed Haidar (16) na baba yake mzazi
Ahmed Haidar Jabir (47) mkazi wa Kiembesamaki ambao wamelazwa katika
hospitali ya Alrahma iliyopo Kilimani na Suleiman Ali Juma ambaye ni
mwanafunzi wa kidato cha sita.
Kwa mujibu wa Kamanda Ilembo waathirika wana
majeraha makubwa, huku mabaki ya vipande vya mabomu vikitolewa kwenye
miili yao. Alisema Khalid Ahmed Haidar ambaye ni mwanafunzi wa kidato
cha tano katika Shule ya Sekondari Light Academic iliyopo Nairobi
ametolewa vipande sita.
“Tumeimarisha ulinzi na usalama katika maeneo
mbalimbali kwa ajili ya kuchukua tahadhari, ikiwamo kufanya doria na
tunawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za siri
zitakazosaidia kuwakamata waliohusika,” alisema DDCI Ilembo.
Akizungumza na gazeti hili katika Hospitali ya
Alrahma, baba wa marehemu Muhammed Khatib Mkombalaguha, alisema alipokea
taarifa za kifo cha mwanaye kupitia kwa ndugu yao anayeishi Arusha na
baadaye alithibitishiwa kutokea kwa tukio hilo baada ya kuwasiliana na
Sheikh Abdulrahman Mussa anayeishi katika eneo la Jitengeni Pongwe,
mkoani Tanga.
“Tulianza safari saa 4:00 usiku kupitia Dar es
Salaam, na saa 12:00 alfajiri tulifanikiwa kufika bandarini na kuanza
safari ya Zanzibar, marehemu ana mke na watoto wawili,” alisema baba wa
marehemu.
0 comments:
Post a Comment