Kama unataka kupata michongo zaidi, kuwavutia watu waje kwenye show yako
au kuuza nyimbo zako, hakuna dawa yoyote unayoweza kuweka kwenye nyimbo
zako. Ingawa kutoa nyimbo nzuri kunasaidia lakini unatakiwa kuwa na
mtazamo na muonekano utakaovutia watu kwa kile unachofanya na pia
kuelewa jinsi mchezo wa biashara ya muziki unavyochezwa.
Haya ni baadhi ya makosa 14 ya mara kwa mara ambayo wasanii wengi hufanya.
1.Kuishi nyuma ya muda katika ulimwengu ambao haukuwa na mitandao ya kijamii
Ujio wa mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter umerahisisha
mawasiliano kwa kiasi kikubwa. Imerahisisha mawasiliano kati ya wasanii
na mashabiki wao au wasanii na vyombo vya habari.
Sentensi fupi kama ‘September 29 ni siku yangu muhimu, ntazindua album
yangu mpya, naombeni support yenu’ kwenye Facebook au Twitter inaweza
kusafiri mamilioni ya maili na kuwafikia mashabiki wako wengi duniani
kote na vyombo vya habari vikapata habari. Bahati mbaya ni kwamba kuna
wasanii wengi wenye allergy na mitandao ya kijamii.
Haijulikani wako wapi, wanafanya nini, wanatoa lini wimbo mpya na kwa
ufupi ni kwamba wamejichimbia shimoni. Kama haupo Facebook, Instagram
wala Twitter, unategemea jina lako liongelewe wapi?
2.Kuanika kila kitu kwenye mitandao ya kijamii
Hakuna haja ya kuandika kwenye Twitter au Facebook kuhusu promoter wa
Kahama aliyeshindwa kukulipa hela yako ya show na ukakosa nauli ya
kurudi Dar es Salaam. Haikusaidii chochote zaidi ya kukushusha. Blogs
zitasherehekea kwakuwa zitakuwa zimepata habari nzuri ya kuvuta traffic
na kukuchoresha zaidi wewe kwa vichwa vya habari kama ‘Ugolo Mweupe
akosa nauli ya kurudi Dar baada ya promoter kumwacha kwenye mataa’.
Wewe ni staa. Unaishi ndoto. Itunze ndoto hiyo. Usimwambie kila mtu
jinsi ulivyopigika na kwamba bado unaishi na mama yako ama kitu chochote
kinachoweza kuharibu heshima kwa mashabiki wako. Kumbuka hauuzi tu
muziki wako bali pia unauza wajihi wako.
3. Kupenda kuponda wasanii wenzako, vyombo vya habari ama wadau wengine hadharani
Kuna wasanii wanaojiona wao ndio kila kitu. Wao ndio rappers ama
waimbaji bora tangu ulimwengu uanze. Mara nyingi tumesikia wasanii
wakihojiwa redioni na kuanza kuponda nyimbo za watu wengine kana kwamba
nyimbo zao zimetungwa kwa msaada wa malaika. Japokuwa una haki ya kutoa
maoni yako pia unapaswa kukumbuka kuwa suala la kukosoa nyimbo hadharani
ni kazi ya wachambuzi wasiofungamana na upande wowote. Unapokosa wimbo
wa mwenzio na kumuita wack mcee, tambua kuwa kuna mashabiki wengi
wanaoumpenda na kwa namna yoyote utakuwa umewakera pia.
Nakumbuka niliwahi kusikia interview ya Hammer Q kwenye kipindi cha Leo
Tena Clouds FM na kumsikia jinsi alivyokuwa akiwadhalilisha madj wa
redio zingine kuwa wanaendekeza rushwa. Japokuwa suala hilo kweli lipo,
lakini hakupaswa kuzungumza hivyo kwenye radio inayosikilizwa nchi
nzima. Nina uhakika siku hiyo alizungumza ujumbe uliowakera watu wa
radio zingine nyingi ambao kuanzia siku hiyo walimuona snitch.
4. Kutokuwa rafiki wa vyombo vya habari
Ni ngumu kuwa karibu na redio, TV, magazeti ama blogs zote nchini lakini
ni muhimu kuziheshimu zote. Ukiombwa interview na kituo cha radio cha
Ludewa, unapaswa kuwa na muitikio sawa na kama unapoombwa interview na
radio kubwa ya Dar es Salaam. Unapokuwa msanii mkubwa, tambua kuwa kila
kona ya nchi kuna mashabiki wako, hivyo usiwanyime fursa mashabiki wako
wa vijijini kujua habari zako.
5. Kuachia nyimbo kwa mfumo wa Exclusive
Niliwahi kuandika mada hii kwa urefu zaidi hapa.
Lakini ninao mfano halisi wa msanii mkubwa aliyeniambia kuwa kipo kituo
kikubwa kimoja cha redio ambacho hakipigi tena nyimbo zake kwasababu
alichagua kwenda kuutambulisha wimbo wake exclusive kwenye kituo kingine
cha redio.
6. Kuwa mikononi mwa meneja asiyekijua kiwanda cha muziki
Asilima kubwa ya wasanii, hasa wachanga wapo chini ya mameneja wenye
pesa lakini wasio na ufahamu wa namna muziki wa Tanzania ulivyo. Wengi
humsaidia msanii kwa kipindi fulani akitegemea matunda yaanze kuonekana
ndani ya miezi mitatu.
Kwa mazingira ya muziki ulivyo Tanzania ni ndoto kupata mafanikio katika
kipindi hicho. Ni bora kuwa na meneja mwenye kipato cha kawaida lakini
anayezijua njia na fitina za muziki wa Tanzania, kuliko kuwa na meneja
mwenye hela lakini anayeishi kwenye ulimwengu tofauti na ule wa muziki.
7. Kufulululiza kutoa nyimbo zinazofanana
Kuna kichaa mmoja alipita sehemu na kuokota noti ya shilingi elfu moja.
Basi kuanzia siku hiyo, alihakikisha anapita eneo hilo zaidi ya mara 20
akitegemea kuwa ataokota tena hela nyingine. Huo ni mfano wa namna
baadhi ya wasanii wa Tanzania walivyo. Wimbo mmoja ukiwa hit, basi
atahakikisha zingine mbili mpya zitakuwa ama na beat inayofanana na ya
mwanzo ama ujumbe/mashairi sawa na wa mwanzo. Kwa mfumo huo, ni ndoto
kufululiza kutoa hits bali utakuwa kama unaachia series au remix za
nyimbo zako.
8. Kutokuwa na producer mmoja anayekupatia
Simaanishi kuwa kila msanii awe na producer mmoja tu wa nyimbo zake.
Maana yangu ni kwamba, kuna namna ambavyo inatokea producer mmoja
humpatia zaidi msanii fulani.
Kwa Tanzania tunafahamu jinsi Mika Mwamba anavyompatia Mad Ice, Mona G
anavyowapatia Young Killa na Belle 9, marehemu Roy alivyokuwa akiwapatia
Mr Blue na Abby Skillz, KGT anavyompatia Ali Kiba, John Mahundi
anavyompatia Crazy GK, P-Funk alivyompatia Jay Mo, Juma Nature na
wengine.
Mfano wa Marekani, Timbaland anavyompatia Justin Timberlake, 40, Matthew
Jehu Samuels Boi-1da na T-Minus wanavyompatia Drake, vocals zote za
nyimbo za Rihanna hufanyiwa kazi (produced) na Makeba Riddick aka Girl
Wonder, nyimbo karibu zote za Jay-Z lazima zipitie mikono ya Rick Rubin
na wengine.
9. Kutafuta Kiki
Kila mmoja anapenda kupata Kiki lakini wakati mwingine Kiki zimewatokea
puani wasanii wengi. Tafuta kile ninachoweza kukiita ‘Intelligent Kick’
na sio ‘Mediocre Kick’.
10. Timing ya kuachia wimbo
Unapofikiria muda wa kuachia wimbo inabidi utulize akili kidogo sababu
unaweza kujikuta ukitupa jiwe gizani. Angalia muda mzuri wa kuachia
wimbo usije ukaachia katika muda ambao wimbo wake utapotea kwenye
rotation baada ya wiki moja tu.
11.Kutojipigia debe
Hivi karibuni nilipiga story na rapper Wakazi na akanieleza jinsi
anavyofanya mambo yake. Kwa kiasi kikubwa jina lake limefahamika kwa
jitihada zake mwenyewe na tena kwa promotion ya online. Alikuwa
akihangaika mwenyewe kujipigia promo kupitia mitandao ya kijamii na
kushirikisha blog zingine. Baada ya kuona watu wengine wa blog
wanambania, akafungua blog yake mwenyewe kibishi na kuandika issue zake.
Ukiwa mmoja wa followers wake, unaweza kugundua kirahisi jinsi
anavyojipromote mwenyewe kwa kuandika tweets kama; Pls Request “Touch”
by Wakazi on your favorite radio station.
Usipojipromote mwenyewe, ni nani mwingine atafanya hivyo?
12. Kulazimisha kushawishi watu wasikie/wacheze wimbo wako
Haina haja ya kulazimisha watu kwa kuwatag Facebook wasikilize nyimbo
zako online. Mara nyingi ukiwa msanii msumbufu wa kuwapigia simu
watangazaji kila siku na meseji zisizo na kichwa wala miguu, unajiweka
cheap na kujishusha.
Kama mtangazaji hajaupenda wimbo wako kwakuwa ni kweli si mzuri,
usijaribu kumshawishi kwasababu, kama ni mbovu hatoucheza. Na kadri
unavyoendelea kumsumbua acheze wimbo wako, ndivyo anavyokumbuka jinsi
ulivyogeuka kero kwake.
Hiyo ina maana kuwa utajiharibia hata kwenye ngoma zako zijazo.
13. Kushindwa kutengeneza uhusiano mzuri na mashabiki wako
Hakuna mtaji mkubwa kama mashabiki. Kama utakuwa na uhusiano nao mzuri,
hawatakuangusha kamwe. Watu si wajinga. Wanafahamu sana pindi unapotaka
wanunue ama wasikilize kazi zako. Kama una uhusiano mzuri na mashabiki
wako na wanajua unawajali watakusupport kwa kila kitu.
Kwenye makala yake aliyoipa jina; ‘6 lessons artists must learn from
‘anacondagate’ Mwandishi na gwiji wa masuala ya Masoko, Constantine
Magavilla aliandika:
Loyal fans outstrip money in the long run so never undermine them. They
will come out and support you when you need them most! The worst thing
you can do is not to appreciate your fans when you are on top of the
world. Remember, your social significance and earnings are a function of
the number fans you have and the value each brings to the table.”
Kila siku – haijalishi upo busy ukirekodi, kwenye tour, au ukiwa
nyumbani na wasiwasi jinsi gani utapata fedha za kufanya video mpya –
fanya kitu (haijalishi kiwe kidogo vipi) kuwafikia mashabiki wako.
14. Kutoa video iliyo chini ya kiwango cha ukubwa wa wimbo
Video inafahamika kwa jinsi inavyoupa uhai wimbo. Kama ukifanya video
nzuri ya hit yako, basi ukubwa wa wimbo utaongezeka mara dufu. Lakini
kama ukifanya video ya kawaida ama iliyo chini ya kiwango cha ukubwa wa
wimbo, video hiyo itaichimbia kaburi refu ngoma hiyo.
0 comments:
Post a Comment