Kanuni za Bunge zawaelemea chama pinzani

Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni wakizuia Kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe (aliyevaa tai ya njano) asitolewe nje ya Ukumbi wa Bunge na Askari wa Bunge baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuamuru atolewe, kwenye kikao kilichofanyia Alhamisi ya wiki iliyopoita, mjini Dodoma.Picha na Fidelis Felix

Dar es Salaam. Kumekuwa na mjadala mkali kuhusu iwapo Naibu Spika, Job Ndugai alikiuka Kanuni za Bunge katika kushughulikia vurugu zilizotokea Bungeni Alhamisi iliyopita kwa kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Ndugai ambaye alikuwa kiongozi wa shughuli za Bunge siku hiyo, aliwaamuru askari kumtoa nje Mbowe baada ya kukaidi amri yake ya kutaka kuketi chini aliposimama kutaka kupewa nafasi ya kuzungumza, hali iliyozua tafrani bungeni.
Pamoja na mambo mengine Ndugai amekuwa akituhumiwa kwamba anaminya uhuru wa wabunge wa upinzani kutokana na mapenzi aliyonayo kwa chama chake, CCM.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na lawama kwamba Mbowe alikosea kukaidi amri ya Naibu Spika kwa kuwa kanuni zinamtaka mbunge yeyote (hata akiwa waziri), kuketi pale kiongozi wa Bunge (Spika, Naibu au Mwenyekiti) anaposimama, hivyo kusababisha mtafaruku.
Mwenyekiti wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, Profesa Chris Peter Maina alisema tatizo lililojitokeza bungeni linaweza kumalizwa na kuwapo kwa sheria inayokataza Spika wa Bunge kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.
“Unajua kwa Katiba ya sasa Spika wa Bunge anaweza kuwa mwadilifu lakini akapata shinikizo kutoka upande wa chama chake, Ibara ya 128 ya Rasimu ya Katiba Mpya inaeleza kiundani kuhusu spika kutokutoka miongoni mwa wabunge jambo ambalo ni zuri,” alisema Profesa Maina na kuongeza:
“Mwenendo wa Bunge siyo mzuri. Wabunge hawaheshimiani hata kidogo, nadhani wanahitaji kukubaliana kwa hoja, wao ndiyo wanatunga sheria, hivyo wanatakiwa kulumbana kwa kufuata utaratibu uliowekwa.”
Spika wa zamani, Pius Msekwa alisema wakati akiongoza Bunge hakuwahi kuona vurugu, fujo na malumbano ya wabunge kama ilivyotokea Alhamisi iliyopita.
“Wakati nikiwa Spika sikumbuki kama kuna siku ziliwahi kutokea vurugu za aina hii, kilichotokea ni sawa na uhalifu kwa sababu taratibu hazikufuatwa,” alisema Msekwa.
Matakwa ya Kanuni
Ibara ya 76 (1) na (2) ya Kanuni za Bunge Toleo la Aprili 2013, zinaeleza jinsi ya kudhibiti fujo bungeni, lakini Ndugai anakosolewa kwamba hakuzingatia taratibu hizo kushughulikia vurugu za Alhamisi.
Kanuni ya 76 (1) inasema: “Kwa madhumuni ya kudhibiti fujo endapo itatokea ndani ya Ukumbi wa Bunge na Spika ataona kuwa kuna haja ya kutumia nguvu, basi anaweza kuahirisha shughuli za Bunge bila ya hoja yoyote kutolewa au kusitisha kikao kwa muda atakaoutaja ili fujo hiyo iweze kudhibitiwa na Mpambe wa Bunge”.
Kadhalika, fasili ya pili ya Kanuni hiyo inasema: “Baada ya utulivu kurudia, Spika atalipeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge suala ambalo lilisababisha kutokea kwa fujo ikiwa ni pamoja na jina la mbunge au majina ya wabunge waliohusika na fujo hiyo ili kamati hiyo iweze kulishauri Bunge kuhusu adhabu inayostahili kutolewa”.
Wakati vurugu zilipozuka bungeni, Ndugai aliwaita askari badala ya mpambe, kumtoa nje Mbowe na hakuwa amesitisha wala kuahirisha shughuli za Bunge kama kanuni zinavyotaka.
Pia Naibu Spika alitangaza kumsamehe Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa maana ya kuwaruhusu kuendelea na vikao vya Bunge siku hiyo jioni, badala ya suala hilo kupelekwa kwenye kamati husika kama kanuni ya 76 (2) inavyoelekeza.
Utetezi wa Ndugai
Ndugai alisema hakuzingatia kanuni hizo kwani mazingira ya vurugu hizo hayaendani na kanuni husika, hivyo alitumia nafasi yake ambayo pia inatambuliwa na kanuni za Bunge.
“Vurugu zilikuwa zimepangwa na zilifanywa kwa makusudi ili kuhakikisha kwamba shughuli za Bunge zinakwama maana hiyo kanuni wanafahamu kwamba ipo, sasa hatuwezi kuwa na Bunge ambalo mtu akiamua tu anafanya fujo ili liahirishwe,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Mimi kama kiongozi wa shughuli za siku hiyo, kazi yangu ni kuhakikisha kwamba shughuli zilizopangwa zinafanyika, kwa hiyo nisingeweza kuruhusu watu wachache watukwamishe kutokana na masilahi yao.”
Alipoulizwa kwamba alifahamu vipi kuwapo kwa njama hizo, alisema kauli na matendo ya wabunge wa upinzani vilionekana tangu mwanzo wa mjadala kutaka kukwamisha shughuli za Bunge siku hiyo.
Kuhusu kuwatangazia wabunge hao msamaha badala ya kupeleka suala hilo kwenye kamati husika, Ndugai alisema: “Hakukuwa na adhabu kubwa ya kuwapa zaidi ya kuwatangazia msamaha.”
“Niliwasamehe kwa mujibu wa kanuni maana zinaruhusu kuzingatia uamuzi ambao uliwahi kutolewa na maspika waliopita, kwa hiyo kama unakumbuka kesi ya Mengi (Regnald) na Malima (Adam), Spika Samuel Sitta baada ya kumwita Malima akakataa kwenda alisema anamsamehe,” alisema na kuongeza:
“Yeye (Sitta) alitumia neno kwamba nimeamua kumpuuza lakini mimi sikusema hivyo, nilisema kwamba namsamehe kwa sababu tu namheshimu na ni kiongozi mkubwa tu katika jamii”.
Lissu amtetea Mbowe
Mbowe hakupatikana juzi na jana kuzungumzia suala hilo, lakini Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema kiongozi wake huyo hakufanya makosa kwani alisimama wakati Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema alipokuwa akizungumza na kwamba hilo siyo kosa kikanuni.
Alisema Ndugai alipaswa kumheshimu Mbowe kwa kuzingatia wadhifa wake bungeni na kwamba kitendo cha kumwambia “kaa chini” hakikubaliki.
“Hatuwezi kuruhusu na hatutaruhusu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kudhalilishwa, ikiwa tutaruhusu hilo litokee, basi miongoni mwetu sisi wapinzani hakuna atakayepona,” alisema Lissu na kuongeza:
“Naibu Spika amelidhalilisha Bunge kwa sababu kwa kumdharau Mbowe ni kwamba amemdharau mmoja wa viongozi wakuu wa Bunge”.
SHARE

Milan Tomic

Hi. I’m Designer of Blog Magic. I’m CEO/Founder of ThemeXpose. I’m Creative Art Director, Web Designer, UI/UX Designer, Interaction Designer, Industrial Designer, Web Developer, Business Enthusiast, StartUp Enthusiast, Speaker, Writer and Photographer. Inspired to make things looks better.

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment