TAARIFA TOKA IKULU JUU YA RAI YA RAIS KIKWETE KWA RAIS BASHIR WA SUDAN


 
Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Sudan Mheshimiwa Omar Bashir kufuatia kuuawa na kujeruhiwa kwa askari wa Tanzania, walioko katika ulinzi wa kimataifa wa amani katika jimbo la Darfur na kumtaka Rais Bashir kuchukua hatua za haraka kuwasaka na kuwakamata waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.

Katika mazungumzo yao, Rais Omar Bashir amekubaliana na Rais Kikwete na kumuahidi kuwasaka hadi kuwakamata wale wote waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria.

Rais Bashir amemueleza Rais Kikwete kuwa binafsi anaamini kuwa waliohusika ni wahalifu na hivyo kuahidi kuwa lazima 

watasakwa hadi kukamatwa kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

Rais Bashir amempa pole Rais Kikwete kwa tukio hilo la kusikitisha ambapo wanajeshi wa Tanzania wameenda nchini Sudan kulinda Amani na Usalama wa wananchi wa Sudan.

Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN) Bw. Ban Ki Moon alimpigia Rais Kikwete na kumpa pole kwa mkasa huo mkubwa na wa kusikitisha ambao umewatokea wa Tanzania hao wakati wakiwa katika kutekeleza jukumu lao la kulinda amani nchini Sudan.

Hadi sasa hakuna kikundi chochote ambacho kimekiri kuhusika na shambulio hilo ingawaje kumekua na kutupiana lawama baina ya vikundi vya kiserikali na vya waasi katika jimbo la Darfur.

Mapigano baina ya vikundi vya kikabila na koo mbalimbali zimesababisha mapigano na uvunjifu mkubwa wa amani na usalama katika jimbo la Darfur kwa muda wa miaka 10 sasa, na mara nyingi mapigano na tofauti zao hizo zimesababisha vifo na uvunjifu wa amani kwa wananchi wa Sudan na wageni pia.

Mwishoni mwa mwaka jana Wanajeshi wanne kutoka Nigeria waliuawa karibu na El Geneina , Magharibi mwa Darfur ambapo pia inaelezwa na Umoja wa Mataifa kuwa wanajeshi wapatao 50 wameuawa tangu kikosi hiki cha Umoja wa Afrika kinachoundwa kwa pamoja chini ya Umoja wa Mataifa (UNAMID) kianze operesheni yake mwishoni mwa mwaka 2007.

Taarifa za Umoja wa Mataifa pia zinaeleza kuwa kabla ya mashambulizi yaliyofanyika dhidi ya kikosi cha Tanzania jumamosi iliyopita, wanajeshi 6 wanaolinda Amani wameuawa tangu oktoba mwaka huu ambapo pia inasadikiwa kuwa watu wapatao 300,000 wameyakimbia makazi yao.

Hata hivyo kiini cha mgogoro huo unaosadikiwa kuwa ni ugomvi wa ardhi na rasilimali zilizoko katika jimbo hilo nchini Sudan.

Miili ya maaskari hao saba wa Tanzania inatarajiwa kuwasili nchini ijumaa tarehe 19, Julai kwa ajili ya maziko.Imetolewa na:

Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu
Dar-Es-Salaam, Tanzania
16 Julai, 2013

SHARE

Milan Tomic

Hi. I’m Designer of Blog Magic. I’m CEO/Founder of ThemeXpose. I’m Creative Art Director, Web Designer, UI/UX Designer, Interaction Designer, Industrial Designer, Web Developer, Business Enthusiast, StartUp Enthusiast, Speaker, Writer and Photographer. Inspired to make things looks better.

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment