Moshi. Zaidi ya wanyamapori 15,220 wameuawa na majangili katika hifadhi mbalimbali zilizopo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) katika kipindi cha miaka minne iliyopita wakiwamo tembo 419.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alipendekeza kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuchunguza kuimarika kwa mtandao wa ujangili nchini.
“Ni mtandao wa kimafia ambao hata baadhi ya
watendaji serikalini wanaujua, lakini wanauogopa sasa. Katika mazingira
haya ni vyema Bunge likachunguza ni kina nani hawa ambao wanaogopwa,”
alisema.
Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Tanapa, Mtango Mtahico, baadhi ya wanyama waliouawa kwa ajili ya kitoweo walikaushwa na kusafirishwa nje ya nchi zikiwamo nchi za Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan.
Mtahico alisema katika wanyamapori hao 15,220 waliouawa na majangili kati ya mwaka 2009 na 2012, kwa ajili ya kitoweo wamo nyumbu, mbogo, nyamera, pofu, pundamilia, swala na wanyama wengine.
Mhifadhi huyo alitoa taarifa hiyo juzi katika kikao cha wadau wa uhifadhi Kanda ya Kaskazini kilichohudhuriwa na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge na wakurugenzi wa halmashauri.
“Ujangili huu wa wanyama ambao unaongezeka nchini unachochewa na mahitaji ya kitoweo na pia mahitaji ya kibiashara kama ya pembe za ndovu na faru duniani”alisema Mhifadhi Mkuu huyo.
Mtahico alisema katika miaka ya hivi
karibuni, mitandao ya ujangili imekuwa ikijiimarisha na kutumia silaha
za kivita, sumu na nyaya ambazo mpaka sasa hazijulikani zinatoka maeneo
gani ya nchi.“Utafiti unaendelea kujua hizi nyaya zinatoka wapi maana
zinakamatwa nyingi, lakini hazipungui na hizi hazichagui zikishategeshwa
zinaweza kuua hata nyumbu 100 kwa mara moja,” alisema Mtahico.
Akizungumza katika mkutano huo wa siku mbili, mbunge wa Karatu, Israel Natse alilalamikia unyama unaofanywa na askari wa Tanapa wanaodhibidi ujangili akitaka wabadili mtazamo wa utendaji kazi.
“Rangers (askari) ni wanyama mno, vitendo wanavyofanya utadhani ni vitendo vile vilivyokuwa vikifanywa na Makaburu,” alisema Natse akilalamikia pia fidia ndogo kwa watu wanauawa na wanyama.
Kauli hiyo iliungwa mkono pia na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari ambaye alisema kuna udhalilishaji mkubwa wanaofanyiwa wananchi wanaokutwa wakiwa ndani ya hifadhi hizo.
0 comments:
Post a Comment