RAIS XI JINPING KUTUWA TANZANIA ZIARA YAKE YA KWANZA TOKA ACHAGURIWE KUWA RAISI


Rais wa China, Xi Jinping 

Fidelis Butahe, Mwananchi
Zikiwa zimepita takribani wiki mbili tangu achaguliwe kuwa rais wa China, Xi Jinping ameichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuitembelea.

Rais huyo anatarajiwa kuwasili leo alasiri jijini Dar es Salaam ambapo atakutana na viongozi mbalimbali nchini, kusaini mikataba ya kidiplomasia 19, ukiwemo wa ujenzi wa Bandari wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Pia atatoa hutuba yake ya kwanza tangu achaguliwe kuwa rais, ambayo itagusia masuala ya kiuchumi, kisiasa sambamba na kueleza msimamo wa nchi yake kwa Tanzania na Afrika.
China ndiyo nchi inayofanya biashara nyingi zaidi na Afrika, kuliko Marekani na nchi za bara la Ulaya na ilianza kushirkiana na Tanzania katika masuala mbalimbali tangu mwaka 1950.

“Uhusiano kati ya China na Afrika ni wa kina”, hiyo ni kauli iliyotolewa na rais huyo siku tano zilizopita ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuanza safari yake kuelekea nchini Urusi.
Ujenzi wa bandari utakaofanywa na Kampuni ya Merchants Holding ya China, utakwenda sambamba na ujenzi wa barabara inayounganisha bandari hiyo na Reli ya Kati na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).

Ujio wa rais huyo umeelezwa kuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania kwani hivi karibuni nchi hiyo imefungua soko la watanzania kuuza tumbaku, sambamba na kuingia mkataba wa kuliendeleza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe juzi aliliambia gazeti hili kwamba Rais Xi pia atafungua jengo la kisasa la mikutano la Mwalimu Nyerere ambalo lilijengwa kwa msaada wa nchi hiyo kwa ajili ya kumbukumbu ya kiongozi huyo.
Akiwa nchini Urusi alizungumza na rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin kuhusu masuala ya nishati na uwekezaji.

Baada ya kutoa hotuba yake kesho alasiri ataondoka kuelekea Afrika Kusini ambako atahudhuria mkutano wa tano wa Brics utakaofanyika Machi 26 na 27.
Brics unajumuisha nchi za Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini zikiwa ni nchi tano muhimu zinazozidi kukua kiuchumi.

Uhusiano kati ya Tanzania na China ulianza zamani tangu enzi za waanzilishi wa mataifa hayo mawili, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Mao Zedong wa China. Moja ya miradi mikubwa ya Uchina iliyofanywa barani Afrika ni ujenzi wa reli ya Tazara ambayo mbali na kuwa ni mradi wa maendeleo pia ilisaidia katika ukombozi wa bara la Afrika, kama moja ya njia za usafiri wakati wa vita.

Mradi mwingine ni ujenzi wa jengo la Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa, Ethiopia.

Xi atafanya mazungumzo la Rais Jakaya Kikwete pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, Xi atafanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein pamoja na kuzindua kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya China kwa lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere.

Baada ya shughuli hizo Xi atatoa hotuba yake itakayojikita kuelezea sera ya Serikali mpya ya China kwa bara la Afrika.
Pia atatembelea makaburi ya wataalamu wa Kichina waliofariki wakati wa ujenzi wa reli ya Tazara yaliyopo Majohe nje kidogo ya mji.

Faida iliyoipata Tanzania kutokana na kuwa na uhusiano na China ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Tazara, Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, Mradi wa Maji Shinyanga, Dar es Salaam na Pwani.
SHARE

Milan Tomic

Hi. I’m Designer of Blog Magic. I’m CEO/Founder of ThemeXpose. I’m Creative Art Director, Web Designer, UI/UX Designer, Interaction Designer, Industrial Designer, Web Developer, Business Enthusiast, StartUp Enthusiast, Speaker, Writer and Photographer. Inspired to make things looks better.

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment