KWA bahati mbaya watu wengi hawatambui kitu kinachofariji,
ndiyo maana wanakimbilia kutegemea msaada. Lakini ukweli ni kwamba mawazo yetu
ndiyo faraja pekee ya maisha.
Tukijikubali, kujipenda na kujiwazia mema hatutafadhaishwa
na hali ya wenzetu kutojali shida zetu, badala yake tutafurahia matatizo yetu
kwa tarajio la “yote yanayopita”.
JE, UNAJUA TOFAUTI YA UBINAFSI NA BINAFSI?
Watu wengi hawafahamu tofauti kati ya maneno haya, kutojua
huko ni msingi wa matatizo ya kimaisha kwa wanadamu wengi na ukosefu wa faraja.
Kama lilivyo jina la kolamu yangu JITAMBUE, watu wengi hawajitambui na kujithamini, ndiyo
maana wanadhani wamezaliwa ili wateseke hapa duniani.
Ni ukweli usiopingika kwamba kila mmoja wetu angejua
kusimama vema kwenye mhimili wa maisha yake tungepunguza kwa kiasi kikubwa
mfadhaiko wa mioyo yetu na msongo wa
mawazo usiokuwa na sababu.
Ifahamike kwamba mwanadamu wa kwanza aliumbwa BINAFSI
(Mwanzo 2:7,”…mtu akawa nafsi hai) Tafsiri ya neno hilo inayopatikana kwenye
kamusi ya Kiswahili Sanifu na TUKI toleo la pili ni “kwa nafsi yangu, kwa ajili yangu mwenyewe tu.” Mwisho wa kunukuu.
Popote pale duniani mwanadamu binafsi ndiye mwenye kuishi kwa furaha, ndiye mwenye mafanikio, anayeweza kujifariji
mwenyewe kwa umaskini wake, hali yake duni, ugonjwa wake sugu, taabu na shida
zake kwa sababu yeye ni mwenyewe tu.
Katika hali ya
kawaida, nyuma ya binafsi kuna ubinafsi ambao unaelezwa kwenye kamusi
“ni hali ya mtu kujifariji na kujipenda yeye mwenyewe” Mwisho wa nukuu ambayo
kwa mtazamo inaelea hewani na kuwafanya wengi wadhani kuwa maana ya maneno haya
ni moja.
Ingawa mimi si mhubiri lakini ni mchunguzaji wa maandiko matakatifu ambayo
yananirudisha kwenye kitabu cha Mwanzo 3:4-5 ambapo nabaini mwanzo wa ubinafsi ulivyoanza kwa
binadamu wa kwanza.
Nukuu ya maandiko hayo inasomeka hivi: Nyoka akamwambia
mwanamke, hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba mtakapokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa
macho nanyi mtakuwa kama Mungu kwa kujua mema na mabaya. Hapa wanadamu hawa wa
kwanza wanatamani kuishi kwa ubinafsi, wanataka kufanana na Mungu wao.
Ubinafsi halisi ninaouzungumzia ndiyo huu, ambao unamfanya
mwanamke ambaye hajazaa atamani kuzaa kama fulani, amiliki gari, awe na maisha
ya juu. Mawazo hayo humsogeza kwenye
hali ya kujidharau na hatimaye kufadhaika.
Hii ndiyo sumu ya ubinafsi ambayo inaua, inadhoofisha
na kuondoa hali ya uthubutu wa
kukabiliana na matatizo yetu kama
wanadamu na kutufanya tulilie kusaidiwa au kufarijiwa na wenzetu.
Msomaji wangu, kuanzia leo fahamu kwamba ukifadhaishwa na
chochote ujue unaumizwa na ubinafsi wako unaokusumbua kutaka uwezo wa mali za
mtu mwingine uwe nazo wewe.
Amini usiamini, mtu mwenye mawazo ya ubinafsi ikitokea
eneo lote analoishi watu wote ni wagonjwa kama yeye, hawajaolewa, hawana
kazi, na maskini, utashangaa kuona
mwanadamu huyo anaishi kwa furaha, si kwa
sababu amefanikiwa, bali amekosa
aliyemzidi wa kujifananisha naye.
Usijiumize kwa kutaka maisha ya mtu fulani yawe yako kwa ghafla.
0 comments:
Post a Comment