Babati. Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, mkoani Manyara, Vrajilal Jituson kupitia Mfuko wa Ofisi yake ameazimia kutoa kompyuta mpakato 28 kwenye maeneo tofauti ya jimbo lake kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi wa taasisi mbalimbali.
Jituson ambaye ni Mwanachama wa Klabu ya Waandishi
wa Habari wa Mkoa huo, (Mamec) alisema alitoa kompyuta mbili mpakato
(Laptop) kwa ajili ya waandishi wa habari wa mkoa huo, ili waweze
kuandika habari za vijijini.
Akizungumza jana mjini Babati, mbele ya Rais wa
Muungano wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Keneth
Simbaya, mbunge huyo alisema amejitolea kompyuta hizo kwa lengo la
kurahisisha teknolojia ya mawasiliano.
“Pamoja na kuwapa waandishi wa habari hizo laptop
mbili pia tumetoa laptop mbilimbili kwenye vituo vya polisi vya mjini
Babati na Magugu ili waweze kusaidia jamii kuandika taarifa zao,”
alisema Jituson.
Alisema katika kompyuta hizo 28, amepanga kugawa
kompyuta tano kwa kila tarafa ili zipelekwe kwenye shule za sekondari,
kwani lengo lake ni kila shule ya sekondari katika kata ipate kompyuta
yake.
Kwa upande wake, Simbaya alipongeza hatua ya
mbunge huyo kugawa kompyuta hizo kwa waandishi wa habari kwani amekuwa
tofauti na wabunge ambao wanawathamini waandishi kwenye kipindi cha
uchaguzi pekee.
0 comments:
Post a Comment