HATA kama ndiyo mara yako ya kwanza kusoma ukurasa huu leo. Lazima kuna kitu kipya ambacho kitaingia ubongoni mwako. Amini maneno yangu, maisha ya wengi yamebadilishwa na safu hii.
Hebu kuwa na furaha maana kuna kitu sasa kinakwenda kufanyika katika maisha yako. Naamini afya yako iko sawasawa na upo tayari kwa ajili ya kujifunza kitu cha tofauti.
Ni mada ambayo ilianza wiki iliyopita. Kwa niliokuwa nao wiki jana, watakumbuka kwamba nilieleza kuwa, kurudiana na mwezi wako wa zamani si dhambi.
Ni suala la moyo wako tu. Moyo ukiridhika, ukikuthibitishia kwamba bado unamhitaji mwenzako, ni jambo jema. Unaweza kuchukua uamuzi wa kutafuta uwezekano wa kutengeneza uhusiano mwingine wenye afya tena. Hapa katika All About Love tunakubaliana na maamuzi ya moyo wako, lakini tunakupa dondoo zitakazokurahisishia kwanza kumpata, lakini pia kujua kama mwenzi wako huyo bado anaweza kuwa wako. Rafiki zangu, kumbuka kwamba, unaweza kuwa na mwenzi, mkapendana kwa dhati na mkadumu kwa muda mrefu lakini kwa bahati mbaya mkaachana kwa sababu ambazo mnazifahamu wenyewe. Katika muda mfupi ambao utakuwa umeachana naye, anaweza kufanya mambo ya ajabu sana. Pamoja na kwamba moyo wako unamhitaji, lakini anaweza kuwa tayari ameshapoteza sifa za kuwa na wewe.
Katika hali hiyo, ni sahihi kurudiana naye? Bila shaka jibu hapa ni siyo sahihi. Siyo sahihi kwa sababu tayari ameshabadilika na si yule uliyekuwa naye awali. Wiki iliyopita tulianza kuangalia kama ni sahihi kurudi kwa mwenzi huyo, faida utakazopata kwa kurudiana naye, kuchunguza sehemu anayopatikana na kufuatilia historia yake baada ya kutengana kwenu. Sasa twende kwenye vipengele vingine.
MAWASILIANO YAKE
Ukishachunguza mahali alipo na kuridhika na historia yake ya kimapenzi baada ya kuachana naye sasa unatakiwa kutafuta mawasiliano yake. Kupata mawasiliano yake ni hatua ya kwanza, kitakachofuata baada ya hapo ni kujenga mawasiliano.
Hapo sasa inategemea na namna mlivyoachana, lakini kama hamkuwa na ugomvi mkubwa sana, basi unaweza kumtumia meseji za kichokozi mara nyingi uwezavyo kwa siku.
Majibu yake ndiyo yatakayokupa mwanga wa kuendelea na kipengele kingine. Kikubwa hapa ni kutozungumzia kabisa mambo ya mapenzi, badala yake iwe ni kumjulia hali na utani wa hapa na pale.
Kwa bahati nzuri siku hizi kuna watu wanatunga meseji zenye vibonzo na kuvunja mbavu. Unaweza kutumia hizo kwa lengo la kumsogeza mwenzako karibu yako wakati ukifikiria kuelekea katika hatua nyingine inayofuata hapa chini.
MWALIKE
Baada ya kutengeneza mawasiliano, sasa unatakiwa kumwalika katika shughuli mbalimbali za kifamilia na binafsi. Mathalani umepata mwaliko wa kwenda kwenye sherehe au hafla fupi ya usiku, omba kampani yake.
Kama mtu mzima atagundua kitu kilichopo moyoni mwako. Hata kama atakuwa mwenye moyo wenye kutu, kutoka naye mbele za watu, kutamfanya akumbuke enzi zenu mlipokuwa mkitoka pamoja, hivyo kufikiria kurudi tena kwako.
Ikiwa ataamua kukuambia kwamba anaona mrudiane litakuwa jambo zuri zaidi, maana atakuwa amekurahisishia lakini akinyamaza, basi njia inayofuata hapa chini ni muafaka kwake.
MVUTE KARIBU YAKO
Sasa unatakiwa kumsogeza karibu zaidi na wewe. Lazima afahamu kwamba, kuna kitu fulani kipo ndani ya moyo wako. Meseji zako zibadilike, kama ulikuwa unamwandikia, “Vp uko poa?” au “Mambo yanaendaje?”, sasa unatakiwa kubadilisha hadi “Niambie sweetie, uko poa?” na kadhalika.
Kwa hakika meseji za aina hiyo zitamfanya aone tofauti na inawezekana kabisa akagundua kwamba upo kwenye mawindo ya kumrudisha tena kwako.
Katika hatua hii katu hutakiwi kufungua mdomo wako kumwambia kuwa unataka kurudiana naye na badala yake unatakiwa kuacha vitendo vizungumze!
Marafiki zangu nawapenda sana na ninatamani sana kuendelea na mada hii lakini kutokana na ufinyu wa nafasi yangu, nalazimika kukomea hapa kwa leo
0 comments:
Post a Comment