
Na Mwandishi Wetu
MWILI wa mwanamuziki Langa Kileo jana (Jumatatu) ulipumzishwa kwenye
nyumba ya milele katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar lakini nyuma ya
kifo chake kuna siri ambayo rafiki yake wa karibu (jina linahifadhiwa)
mkazi wa Mikocheni A jijini Dar ameamua kuiweka hadharani.
Akizungumza na Uwazi juzi, rafiki huyo wa marehemu alisema, siku chache
kabla ya kifo chake alimfuata na kumwambia kuwa Israel mtoa roho
anamtembelea usiku na anahisi siku si nyingi atamfuata mshikaji wake
aliyetangulia mbele ya haki, Albert Mangweha ‘Ngwea’.
“Hii ni siri ambayo hata ndugu zake hawaijui lakini mshikaji alijua
anakufa. Alijitahidi kukikwepa kifo lakini alishindwa. Siku chache kabla
hajafa, usiku alikuja kwangu na kuniambia kule kwao kwenye geto lake
analoishi ambalo liko ghorofani, anaona mauzauza na anahisi kifo
kinamuita.
“Nilishangazwa sana na maneno yale. Akazidi kuniambia eti kwa jinsi
mambo yanavyokwenda hawezi kuendelea kulala kwao na kuanzia siku ile
angelala na mshikaji wetu mwingine pale Geza, Mikocheni A.
“Kweli siku hiyo alilala pale akiwa na hofu kubwa na asubuhi baadhi ya
watu wakawa wanamshangaa akiwa ‘amezima’ nje ya lile geto la mshikaji
wake. Alivyoondoka sikumuona tena mpaka nilipokuja kuambiwa yuko hoi kwa
malaria na kesho yake nikasikia hatunaye, nimeumia sana,” alisema mtoa
habari huyo.
Alipoulizwa juu ya uhusiano wa kifo cha Langa na matumizi ya madawa ya
kulevya, rafiki huyo alisema: “Inaweza ikawa ngumu kwa ndugu wa marehemu
kuhusisha kifo chake na madawa ya kulevya lakini mimi namjua Langa nje
ndani, ukweli ni kwamba jamaa alikuwa akiendelea kula ‘mambo’.
“Alikuwa anakuja maskani tunakula mambo yetu na hata wakati anafanya
kazi kwenye ile Kampuni ya Barrick hapa Dar, ilikuwa kabla hajaenda
anapita kwanza huku uswahilini kisha ndiyo anaenda. Kwa maana hiyo
malaria ndiyo iliyomuua lakini hata madawa yamechangia.”
Langa alifariki dunia Juni 13, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili jijini Dar. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amini!
SORCE: Globalpublishers
0 comments:
Post a Comment