Lukuvi amchefua Mbowe


  *Ashangazwa na kauli aliyotoa bungeni
  *Mtupa bomu adaiwa kubebwa na Polis
Taarifa ya serikali iliyosomwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kuhusiana na tukio la shambulizi la bomu jijini Arusha Jumamosi iliyopita, imemchafua Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Pamoja na kulaani tukio hilo, Lukuvi aliwahusisha wanasiasa ambao hakuwataja kwa majina kuwa wanahusika katika kufanya uchochezi na kuwajaza wananchi chuki.
Alisema kuwa polisi waliokuwapo katika mkutano wa Chadema baada ya kurushwa kwa bomu, walitaka kumfuatilia mhusika, lakini walishindwa na kuamua kujihami baada ya wananchi kuwanza kuwashambulia.
 
Mbowe akizungumza jana jijini Arusha, alisema kuwa chama chake kinao ushahidi wa picha  zinazoonyesha jinsi Polisi walivyoshiriki kutekeleza amri ya Chama  Cha Mapinduzi  (CCM).
 
Alisema kuwa kutokana na kuibuka maneno ya kupotosha yanayotolewa na viongozi wa serikali ili kuficha ukweli wa tukio hilo, watalazimika kuanika mambo yote hadharani.
“Kama Waziri anatoa kauli za namna hii kuwa vyama vya siasa ndiyo wahusika wa kuchochea wananchi, wakati ukweli unaonekana nimemshangaa sana, na serikali inajua ukweli wa hili na hata wakificha tutaenda hata nje kutafuta ukweli,” alisema.
 
Alisema kuwa tukio hilo ni la kupangwa na serikali kwa kuratibiwa na Jeshi la Polisi, kwa sababu hata Spika wa Bunge, Anne Makinda, haja mpigia simu kumpa pole kama Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa kunusurika kuuawa pia kwa Watanzania waliouawa.
 
“Hii inaonyesha jinsi gani tukio hili limepangwa na tumefanyiwa hivi, nchi nzima magari yetu yamevunjwa na kuharibiwa vibaya na hata Mbunge wetu wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, amepigwa katika Jimbo la Edward Lowassa na kundi la CCM,” alisema.
 
Mbowe alisema kuwa anashangazwa kuona Polisi wako mstari wa mbele kuchunguza tukio hilo la mauaji wakati wao ni waratibu wa tukio hilo.
 
Alisema wapo watu waliofanikiwa kuwaona warushaji na walipokimbia kuingia katika gari na kuwa walifuatiliwa na kuona wanashushwa Polisi kwenye gari la Toyota Land Cruiser la rangi ya bluu, likisindikizwa na gari la Land Rover.
 
 “Katika gari aliloingia mhalifu, walikuwamo Polisi wawili hadi walipofika kituoni Polisi na kumshusha aliyelipua bomu hilo,” alisema.
Alisema katika hali ya kawaida alitarajia shughuli za Bunge zisimame kwa ajili ya msiba huo, lakini mambo yakawa tofauti  na watu walivyozoea.
 
“Lakini cha kushangaza Polisi wamekamata watu watatu wa Chadema na wanawatesa ili waonyeshe picha za video walizochukua, wakati wao siyo wahusika wala hawajui kitu, wanawaonea bure,” alisema.
 
Alisema kama hali ni hiyo ya umwagaji damu, ni bora mfumo wa vyama vingi ufutwe umma ujue moja kuliko kuhadaa ulimwengu kuwa kuna vyama vingi wakati ni kiini macho.
 
Mbowe alisema hata Nassari alipokuwa akipigwa, Lema alikuwa na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja, akampa simu asikilize ili atoe maagizo kwa Polisi Monduli kumsaidia Mbunge huyo, lakini Chagonja aliweka simu pembeni na hakutaka kuongea na simu hiyo.
 
Alisema kutokana na hali hiyo wao wataendelea na harakati zao za kisiasa hata kama watauawa na kuwa wanaamini kuwa chama kitaendelea kwa sababu chama siyo Lema wala Mbowe.
 
Kuhusu kauli ya Lukuvi kwamba siku ya tukio Polisi walisaidia kuwaokoa watu, alikataa na kusema kuwa hakuwapo
hata mmoja aliyemnyanyua mtu kumpeleka hospitalini, hivyo huo ni uongo.
 
“Majeruhi wengi walioko hospitalini wana majeraha ya bastola na hata marehemu aliyefariki siku ya kwanza  Ramadhani Juma aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani,” alisema.

IDADI YA VIFO YAONGEZEKA
 
Idadi ya vifo imeongezeka na kufikia watatu, baada ya Amiri Ally (9) kufariki dunia jana akiwa kwenye hospitali ya Selian.
 
Mkurugenzi wa Hospitali ya Selian, Dk. Paul Kisanga, alithibitisha kuwa Amir alikutwa na mauti akiwa amelezwa katika wodi ya wagonjwa wenye uangalizi maalum (ICU).
 
HALI YA NASSARI
 
Pia Mbowe alisema hali ya Nassari siyo nzuri kwa sababu bado anahitaji vipimo zaidi na kwamba madaktari kutoka Hospitali ya Muhimbili, Kitengo cha Mifupa (MOI) watakwenda kumfanyia uchunguzi zaidi kwa kushirikiana na
madaktari wa hospitali hiyo.
 
Akizungumza kwa tabu, Nassari alisema kuwa alizingirwa na watu zaidi ya 40 wakiwapo Wasomali watatu, waliokuwa wakimpiga kwa marungu na kilichomwokoa ni bastola aliyokuwa nayo.
 
“Hawa watu walikuwa na nia ya kuniua kwa sababu walikuwa wakinishambulia zaidi kifuani, chini ya shingo na kichwani kwa kunipiga na marungu kama mwizi, nilipoona hali mbaya nikajitahidi kukimbilia kwenye gari langu na kutoa bastola yangu wakakimbia,” alisema.
Nassari alisema kundi la watu waliomshambulia alibahatika kuwatambua watu wawili ambao ni wakazi wa Wilaya ya Arumeru.

WAWILI WAHAMISHIWA NAIROBI
 
Dk. Kisanga alisema wagonjwa wawili ambao ni Fatuma Jumanne na Sharifa Jumanne walikimbizwa jijini Nairobi, Kenya kwa matibabu. Wote ni wa familia moja.
 
KATIBU WA LEMA HOI
 
Aidha, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, Gabriel Lucas, hali yake imebadilika na yupo ICU na kufanya idadi ya majeruhi walioko ICU kuwa wawili akiwamo Fahad Jamal (7).
 
MAJERUHI ASIMULIA
 
Mmoja wa majeruhi alioko hospitalini hapo, Abdallah Alila (39), alisema ameumia vibaya mguuni baada ya kupigwa risasi na askari polisi na mguu mwingine kudondokewa na vipande vya bomu.
 
“Mimi nilikuwa nyuma ya jukwaa kuu nikimtazama Mbowe, alipomaliza kutoa hutuba akashuka jukwaani na kukusanya sadaka, ndipo nilipoona mfuko wa rambo mweusi mdogo unapeperuka juu, tukadhani upepo unapeperusha, ghafla ulipotua tukasikia kishindo na akasika mama mmoja apiga kelele kuwa aliyerusha anakimbia yule, nilipogeuka nikajikuta nimenguka chini,” alisema.
 
 “Lakini mwisho wa yote kijana aliyerusha hilo fuko aliingia katika gari la Polisi na kuondoka mahali hapo kwa kasi, mimi nilikuwa chini wakati huo naangalia kila upande,” alisema.
 
Alisema alikuwa ameangukia katika mtaro na watu waofika kutaka kumuokoa, aliwambia waondoke wajiokoe mwenyewe.

POLISI WATUPIWA LAWAMA
 
Baba mzazi wa marehemu Ramadhani Juma aliyeuawa katika ugaidi huo, Juma Ramadhani, alisema kuwa anashangazwa kuona jopo la askari wapelelezi wakifika nyumbani kwake Mianzini na kumtaka kukubali kutoa mwili wa mtoto wake bila uchunguzi ili usafirishwe kwenda kwao Tabora kwa mazishi.
 
“Hawa watu nashangaa wanadai kuna magari yapo manne kuwa nitapelekwa nyumbani, lakini nimekataa kwa sababu wanadai nisikubali Chadema kuhusika katika msiba huu, mimi sikubaliani nao kwa kuwa Mbowe alinisaidia mwanzo wa tukio hadi mwisho alipofariki mikononi mwake,” alisema.
 
Alisema hawezi kumwacha Mbowe kwa kuwa ni msimamizi wake katika hatua zote.
 
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, jana hakupatikana kuzungumzia madai hayo.
 
Kila alipopigiwa simu ya mkononi hakuipokea.
 
SERIKALI YATANGAZA BINGO
Serikali imetangaza bingo ya Sh. milioni 100 kama zawadi kwa watu au mtu atakayefanikisha kunaswa kwa mhalifu wa matukio ya ulipuaji mabomu na mtandao wake.
 
Akifafanua Lukuvi alisema mtu atakayefanikisha hilo atapewa Sh. milioni 10 fedha ambazo zitaendelea kutolewa kwa kila mtu na kama zitakuwa zimemalizika basi serikali itatenga fedha nyingine.
 
DK: BILALI: WAHUSIKA WATAKAMATWA
 
Serikali imesema kuwa itafanya  kila jitihada kuhakikisha  kuwa waliohusika katika tukio la ulipuaji wa bomu hilo watatiwa mbarano na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alipowatembelea waathirika.
 
Alisema kuwa  serikali imepokea kwa masikitiko makubwa tukio hilo ambalo ni la kigaidi na kwamba haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote aliyehusika na tukio hilo iwapo atakamatwa.
 
Aliwataka wananchi wavute subira, wawe wastamilivu  na wavumilivu hususani katika kipindi hichi ambacho upelelezi unaendelea.
 
“Napenda kuwaambia msikate tama, vuteni subira kwani  aliyehusika atakamatwa tu hata kama ikitumia muda wa siku tatu, siku kumi mwezi na hata miaka mitatu na zaidi lakini aliyefanya tukio hili atakamatwa tu hata akienda wapi, ninachopenda kuwaambia wananchi kuwa mjenge imani na
serikali yenu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na mshirikiane a mwishowe matatizo haya yatakwisha,”  alisema Dk. Bilal.
 

MAREKANI YALAANI 
 
Marekani kupitia ubalozi wake nchini, imelaani vikali  tukio hilo.
 
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt, alisema Marekani imelaani vikali tukio hilo la kusikitisha na kwamba inatoa salamu za pole kwa familia zilizopotelewa na ndugu zao na majeruhi kwenye tukio hilo la kusikitisha. 
 
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, tukio hilo la juzi linafuatia lile lililotokea Mei 5, mwaka huu katika Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph, jijini humo ambalo liliua watu watatu na kujeruhi zaidi ya 60.
 
Serikali ya Marekani imetoa wito wa kukamatwa, kushitakiwa na kisha kuhukumiwa kwa wote waliohusika na tukio hilo la kusikitisha.
 
Alisema Tanzania ni nchi ambayo inajulikana toka zamani kwa utajiri iliyonao wa utamaduni, uvumilivu na tofauti mblimbali lakini vitendo kama hivyo vinataka kuitia doa, kutishia amani na usalama wa nchi hii iliyojaliwa kuwa na ardhi kubwa.
 
Alfonso aliongeza kuwa, Marekani inasimama kama rafiki wa karibu kwa Watanzana wote na kuwataka kupinga vitendo hivyo vinavyofanwya na baadhi ya watu wanaojaribu kutishia usalama wao.
 
Pia Marekani ilitoa wito kwa raia wote wa Tanzania kudumisha umoja, hekima na amani vilivyoachwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
 
 
TEC YALAAMI
 
Askofu wa Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC), ambaye pia ni  Askofu Mkuu wa Jimbo  Katoliki la Iringa, Tarcius Ngalalekumtwa, alisema kuwa Baraza hilo linalaani tukio hilo la kinyama kwa nguvu zote.
Askofu Ngalalekumtwa alisema kuwa kiongozi wa dini anapotoa kauli ya kulaani basi kauli hiyo inatoka moja kwa moja kwa Mungu.
 
MUFTI: TUTAJADILI
Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban Bin Simba, alisema kuwa tukio hilo haliwezi kutolewa tamko , kwani inabidi akutane kwanza na Masheikh ili walizungumzie kwa kina ili wapate kulitolea tamko kali.
 
Alisema kwamba alikuwa anafanya utaratibu wa kukutana na Masheikh hao ili wazungumze na kuongeza kuwa hakuna kiongozi yoyote wa dini atakayelifurahia, na kwamba  kiongozi yeyote atakayelifurahia tukio kama hilo basi huyo siyo kiongozi.
LHRC: POLISI WADHIBITI SILAHA
Polisi wametakiwa kudhibiti uzagaaji wa silaha ili kuepusha matumizi yasiyo sahihi kwa kuteketeza maisha ya raia wasio na hatia.
Mtafiti wa masuala ya haki za binadamu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Pasience Mlowe, alisema:
 
“Tumesikitishwa sana na tukio hili kwani ni la pili kwa kipindi kifupi kwenye mkoa huo huo, kama watetezi wa haki za binadamu, tunalitaka Jeshi la Polisi kudhibiti uzagaaji wa silaha, hizi si bidhaa zinazoweza kuuzwa ovyo na kila mtu kuwa nazo,” alisema.
 
Alisema iwapo silaha zitaachwa ziingie kwenye mikoni ya raia kirahisi, kuna hatari ya watu kuuawa na kujeruhiwa kila mara na kuonekana ni jambo la kawaida.
 
Aidha, Mlowe aliwataka wanasiasa kuepuka siasa za chuki zinazotengeneza sumu miongoni mwa wananchi na badala yake wajinadi kwa sera za vyama vyao na rasilimali za nchi.

TCD KUKUTANA KUJADILI
Kitio cha Demokrasia Tanzania (TCD),  kitakutana mwezi ujao kutafakari kwa pamoja amani ya Taifa  ikiwemo tukio la mlipuko huo.
 
Mwenyekiti wa TCD,  James Mbatia, alisema jana mjini Dodoma kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya uvunjifu wa amani ikiwemo mauaji ya watu wenye ulemavu, kwa sababu za kishirikina na mauaji ya watu mbalimbali.
 
Aliyataja matukio hayo kuwa ni pamoja na viongozi wa dini, uchomaji wa makanisa, kukashifu na kukejeli dini watu wengine, machafuko ya kutoridhika na matokeo ya chaguzi na migogoro ya ardhi na raia kuuawa askari wa jeshi la polisi na polisi kuuawa na raia.
 
Mbatia alisema licha ya matukio hayo kuwa na athari katika usalama wa taifa, pia yanaweza kusababisha kupunguza mapato nchini yanayotokana na watalii na kuhoji kuhusiana na majibu mepesi ya serikali kuhusiana na matukio hayo.

NAPE ADAI CHADEMA INAHUSIKA
Chama Cha Mapinduzi, (CCM) kimelaani tukio hilo na kudai kuwa Chadema ndiyo wanahusika kutokana na dalili na mazingira yaliyokuwepo.
 
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho, Nape Nnauye, alisema CCM inalaani tukio hilo na matukio mengine yanayofanana na hayo yaliyotokea nchini.
 
Alisema kuwa Chadema kinataka umaarufu kupitia matukio na majanga na kwamba wao ndio wanahusika na urushaji wa bomu hilo kwani kabla ya kufanyika uchaguzi wa kata, walishasema kama hali ikiwa mbaya kwa gharama yeyote watahahakikisha uchaguzi wa madiwani katika Mkoa wa Arusha unaahirishwa.
 
Hata hivyo, hakuonyesha ushahidi wowote wala kuahidi kuwasilisha ushahidi huo ili kulisaidia Jeshi la Polisi.
SHARE

Milan Tomic

Hi. I’m Designer of Blog Magic. I’m CEO/Founder of ThemeXpose. I’m Creative Art Director, Web Designer, UI/UX Designer, Interaction Designer, Industrial Designer, Web Developer, Business Enthusiast, StartUp Enthusiast, Speaker, Writer and Photographer. Inspired to make things looks better.

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment