Nchi yakumbwa na hofu ya kutokuwepo kwa usalama kutokana na kesi inayoendelea
Nairobi. Marekani imetoa onyo kwa
raia wake wanaoishi Kenya wajiepushe na mikusanyiko ya umma kutokana na
uwezekano mkubwa wa kuzuka kwa ghasia zitakazotokana na uamuzi wa
Mahakama ya Juu unaotarajiwa Jumamosi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ubalozi huo
Nairobi, Serikali ya Marekani iliwaonya raia wake dhidi ya kukaribia
mikusanyiko ya watu na kuepuka maandamano na kuacha kukaa katika
maeneo ya kibiashara yasiyo katikati mwa jiji na mitaa.
Taarifa hiyo ilisema kwamba wakati wowote
panaweza kutokea ghasia wakati Mahakama ya Juu inatarajiwa kutoa uamuzi
wa kesi zinazopinga matokeo ya uchaguzi wa urais ifikapo Machi 30.
Huenda kukawa na hisia kali kutoka kwa umma
kutokana na uamuzi utakaotolewa,” taarifa hiyo iliyowekwa kwenye tovuti
yao Jumatatu ilisema.
“Kumbuka pia mikusanyiko inayonuiwa kuwa ya amani
inaweza kugeuka na kuwa ghasia kwa ghafla.” Taarifa hiyo ilizidi kusema
kutokana na kuwa uamuzi huo utatolewa wiki ya Pasaka, wanaosafiri kwa
mapumziko wanafaa kujitahadhari kwa kuwa huenda kukashuhudiwa
misongamano ya magari iwapo ghasia zitaibuka.
“Maandamano huenda yakasababisha misongamano ya
magari na kufungwa kwa barabara. Raia wa Marekani wanashauriwa
kufuatilia matangazo ya vyombo vya habari nchini ili wapate maelezo
jinsi yanavyochipuka kuhusu maandamano na matatizo ya trafiki.”
Mahakama ya Juu inatarajiwa kutoa uamuzi wake
kuhusu iwapo kulikuwa na haki katika matokeo ya uchaguzi wa urais
yaliyotangazwa wiki mbili zilizopita na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka
(IEBC), ambapo Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi.
Kiongozi huyo wa TNA, aliye kwenye muungano wa
Jubilee, alitangazwa mshindi Machi 9, baada ya kupata kura 6,173,433
dhidi ya kura 5,340,546 za Odinga.
0 comments:
Post a Comment