
Mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, amekibebesha Chama Cha
Mapinduzi (CCM) vurugu na mauaji ya kidini huku akiwaonya viongozi wa
Chadema watakaoshiriki na kuhamasisha chuki dhidi ya dini nyingine kuwa
watafukuzwa kwenye chama hicho asubuhi na mapema.
“Udini ni sera ya CCM, wamelikoroga, sasa tunataka walinywe,” alisema
jana wakati akifungua mkutano wa viongozi wa majimbo 33 na mikoa ya
Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro
na Tanga, ikiwa ni sera yao ya majimbo.
Pamoja na kuwaonya viongozi, Mbowe pia aliwataka wanachama wa Chadema
popote pale walipo wasishiriki kuwabagua wenzao kwa imani ya dini bali
waheshimu imani za watu wengine.
Aidha Mbowe alisema; “Chadema inalaani vikali mauaji ya viongizi wa dini
yanayotokea maeneo mbalimbali nchini…tunaitaka CCM na serikali yake
kuwajibika dhidi ya mauaji hayo.”
“Kuona kiongozi wa dini akimwagiwa tindikali, akipigwa na hata kuuawa
kwa sababu za kidini sio mambo ya kujivunia hata kidogo…CCM ndiyo
iliyokuwa ikilea udini na hapo ndipo ilipotufikisha…tunataka CCM na
serikali yake iwajibike kwa hilo.”
Alisema Mkristu hana haki ya kumhukumu Mwislamu na wala Mwislamu hana
haki ya kumhukumu Mkristu, hivyo Chadema kimeamua kuchukua hatua kali
dhidi ya mwanachama ye yote bila kujali wadhifa wake atakayehamasisha
chuki za kidini.
Alisema sera ya udini iliaasisiwa na CCM kama mbinu yao ya kuwafanya
waendelee kubakia madarakani lakini hali inavyoonekana sasa inatisha
amani na umoja wa taifa.
0 comments:
Post a Comment